Mahakama ya Katiba nchini Uganda leo imeidhinisha mabadiliko ya katiba yanayoondoa kikomo kwa umri wa ugombea urais nchini humo.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Julai 27, katika Mahakama Kuu huko Mbale na Naibu Jaji Mkuu, Alfonse Owiny-Dollo, ambaye alianza kwa kuomba radhi kwa mahakama kuchelewa kuanza katika muda uliopangwa awali.
Mahakama ilitakiwa kuyatolea maamuzi masuala makuu matatu ambayo ni kuondolewa kwa kikomo cha umri wa mgombea urais, kuongezwa muda wa kuhudumu bunge na vurugu zilizotokea bungeni mwaka jana.
Hata hivyo, mahakama imekataa kuongeza miaka ya wabunge waliotaka kusalia madarakani kwa miaka saba badala ya mitano ya sasa.
Katika uamuzi, wake Jaji Cheborion Barishaki ameeleza kwamba kuongezwa kwa muhula wa kuhudumu bunge kutoka miaka mitano hadi miaka saba itakuwa ni hatua ya kibinfasi na inakwenda kinyume na maadili ya uongozi bora
Mjadala huu ulianzia bungeni ambapo ulijadiliwa kwa siku tatu na kuleta mvutano baina ya wabunge wa nchi hiyo hadi kufikia hatua ya kupitisha muswada huo wa kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75 kwa ugombea urais baada ya upinzani kupata kura 62.
Hata hivyo, waliotaka kuondoa ukomo umri wa urais kura walipata kura 315 na wawili kutofungamana na upande wowote na kusababisha Spika wa Bunge hilo, Rebecca Kadaga kutangaza kuwa muswada huo umepitishwa baada ya kusomwa mara tatu.
Awali, umri wa mwisho kwa kugombea urais nchini humo, ulikuwa ni miaka 75. Kwa uamuzi huu wa mahakama ina maana kuwa Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni atakuwa huru kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021.