JESHI la Polisi wilayani Nkasi mkoani Rukwa linamsaka Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, Eradi Kapyela anayedaiwa kuikimbia shule yake akituhumiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wake wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 14 .
Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi ipo katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Kata ya Kala wilayani Nkasi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Missana Kwagula alikiri kutaarifiwa juu ya mkasa huo huku akiongeza kuwa siku nne zimepita tangu Mwalimu Mkuu huyo alipotoweka shuleni kwake bila taarifa ili kukwepa mkono wa sheria.
Jitihada zinaendelea za kumsaka Mwalimu Mkuu huyo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alieleza gazeti hili kwa njia ya simu akithibitisha kuwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nkasi linamsaka mwalimu huyo huku akiapa kuwa lazima atatiwa nguvuni ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na iwe fundisho kwa walimu wenzake.
Mbunge wa Nkasi Kusini, Deusderius Mipata (CCM) aliibua hilo katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi jana katika Mji mdogo wa Namanyere huku akishangazwa na kitendo cha serikali wilaya kulifumbia macho kwa kutomchukulia hatua yoyote mwalimu mkuu huyo.
"Mimba shuleni katika wilaya yetu bado ni changamoto kubwa hivyo jitihada za mapambano hayo ni lazima ziendelee...Mwalimu Mkuu Kapyela lazima asakwe, atiwe nguvuni kisha afikishwe mahakamani ,"amesema.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nkasi (DAS), Festo Chonya alikiri kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya inazo taarifa hizo kwamba zinafanyiwa kazi huku akisisitiza kuwa lazima Mwalimu Mkuu huyo atakamatwa hata kama akikimbia kusikojulikana kwamba Serikali ina mkono mrefu.
"Serikali ya wilaya hii, ipo makini sana juu ya hilo na kuwa mapambano hayo yamekua yakififishwa na wananchi wenyewe kwa kushindwa kutoa ushahidi wa kutosha mahakamani na kuwataka madiwani kuwahamasisha kutoa ushirikiano kwa Serikali pale kesi hizo zinapofikishwa mahakamani," amesema.
Diwani wa Kata ya Kabwe, Ahsante Lubisha (Chadema) amesema kuwa licha ya wao kuwakamata wanaume wanaowapatia wanafunzi ujauzito bado wengi wao wanashinda kesi wanapofikishwa mahakamani huku akiishauri serikali kuliangalia hilo kwa kina.
Chanzo- Habarileo