Mwanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Kagoma wilayani Muleba mkoani Kagera (jina tunahifadhi) anadaiwa kubakwa leo asubuhi wakati akielekea shuleni.
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kagoma, Patrick Luhosho amesema mtuhumiwa amekamatwa na anahojiwa akihusishwa na tukio hilo.
Luhosho amesema inasemekana mtuhumiwa alimuita mwanafunzi na kuingia naye ndani ya nyumba ambapo watu waliofuatilia walizingira nyumba na kumkuta amemshikilia mwanafunzi ambapo walimkamata kumfikisha ofisi ya kijiji.
"Niliona wanataka kumdhuru nikaita polisi kuomba msaada wa kiusalama, niliyempigia alikuwa njiani akienda Muleba mjini ndipo wakamchukua kwa ajili ya kuhojiwa," amesema Luhosho.
Mzazi wa mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) amesema kwa sasa yuko katika zahanati akisubiri binti yake afanyiwe uchunguzi.
"Muda huu niko Zahanati ya Izigo na askari polisi nasubiria majibu ya mganga, kitakachobainika nitakupigia kukwambia nilichoelezwa ikiwemo hali ya mtoto kiafya," amesema.
Baadhi ya mashuhuda wamesema mtuhumiwa ni mfanyabiashara wa bidhaa ndogondogo za duka na inadaiwa alipohojiwa na wananchi alidai alikuwa akimpatia mwanafunzi huyo vifaa vya shule.
Na Shaaban Ndyamukama,Mwananchi