Hatimaye aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Lameck Nchemba, amekabidhi ofisi kwa waziri Kangi Lugola. Makabidhiano hayo yamefanyika mapema leo asubuhi kwenye makao makuu ya wizara hiyo yaliyopo jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwigulu amesema kuwa anamtakia majukumu mema Lugola katika utumishi wake kwa watanzania na kuongeza kuwa mbali na kukabidhi ofisi, amekabidhi pia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambayo ina majukumu yaliyopo mbele yake kwa sasa.
“Mbali na ofisi nimekabidhi pia hotuba ambayo ndiyo yenye majukumu ambayo yalikuwa yamepangiliwa kama wizara na serikali katika bajeti hii na kikubwa ni mabadiliko ya baadhi ya sheria zilizokuwa na mapungufu hasa kwa Jeshi la Polisi”, amesema Mwigulu.
Mwigulu ametaja moja kati ya majukumu aliyoacha mezani kuwa ni,kupunguziwa faini kwa madereva bodaboda na bajaji iwe tofauti na madereva wa magari makubwa kwani kuwekwa kwa kiwango sawa ni uonevu kwa madereva hao.
Social Plugin