Getayawkal Ayele: 'Nabii' wa Ethiopia aliyejaribu kumfufua mfu
Maafisa wa polisi nchini Ethiopia wamemkamata kijana mmoja anayejiita 'nabii' kwa jina Getayawkal Ayele baada ya kushindwa kumfufua mfu aliyefariki siku nne zilizopita.
Tukio hilo limetokea katika mji wa Galilee huko Wollega magharibi mwa Ethiopia.
Kanda ya video ya 'nabii' huyo ikiita jina la mfu huyo kwa lengo la kumfufua ilisambazwa sana katika mtandao wa facebook.
Kanda hiyo ya video inaonyesha 'nabii' huyo akilala kando ya mwili huo na kuita jina la marehemu.
Awali alikuwa amekwenda kwa familia ya mfu huyo kwa jina Belay Bifu na kuwahubiria kuhusu habari ya Lazurus, vile Yesu alivyomfufua, muhubiri kutoka mji wa Dhinsa Dabela aliambia BBC.
''Niliona watu wengi wakikimbia kuelekea kule kaburi hilo lilikokuwa wakisema Belay anakaribia kufufuka. Niliwashauri watu kutomuamini nabii huyo lakini walinifukuza wakisema sina imani'', muhubiri huyo alisema.
Nabii huyo baadaye aliwafanya watu kuchimba kaburi , na kuchukua kipande cha nguo kilichotumika kumfunga marehemu na kuanza kumwambia Belay amka tena na tena.
Baada ya majaribio kadhaa ambayo hayakufanikiwa nabiii huyo aliondoka katika kaburi hilo akisema haiwezekani.
Wanachama kadhaa wa familia walikuwa wagonjwa huku wengine karibia wazirai hapo hapo Dhinsa alisema.
Watu waliokuwa wakitazama kisa hicho walikasirika na kuanza kumpiga kabla ya polisi kuwasili na kumkamata.
Kamanda wa polisi katika eneo hilo Tadese Amenu alithibitisha kwa BBC kwamba nabii huyo anazuiliwa na maafisa wa polisi.
Kulingana na kamanda huyo nabii huyo aliyegunduliwa kuwa mfanyikazi wa afisi ya idara ya afya na hakuwa mwanachama wa kanisa lolote.
Social Plugin