Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI NDUGULILE AHIMIZA WAJAWAZITO KUJIFUNGULIA KATIKA VITUO VYA AFYA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ametoa wito kwa akina mama wajawazito kuona umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo Julai 22,2018 katika nyakati tofauti wakati akiwa katika ziara yake katika Wilaya ya Bariadi na Itilima mkoani Simiyu.

Amesema Serikali imefanya jitihada kubwa katika kujenga vituo vya kutolea huduma za afya, majengo ya upasuaji na wodi za wazazi hivyo ni vema wananchi wakatumia vituo hivyo ili idadi ya wanawake wanaojifungulia majumbani ipungue na idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi pia iendelee kupungua.

“Huduma tumewasogezea karibu mzitumie, hususani wakina mama wajawazito, ujauzito siyo ugonjwa na wala mwanamke hatakiwi kufariki sababu ya ujauzito, tuhakikishe wakina mama wanahudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma, tunataka vifo vya akina mama na watoto viwe historia” alisema Dk. Ndugulile.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akisoma taarifa ya Mkoa kwa Naibu waziri, amesema idadi ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya imeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 2016 na kufikia asilimia 81 mwaka 2017, huku idadi ya vifo ikiongezeka kufikia vifo 48 kutokana na sababu mbalimbali.

Kutokana na takwimu kuonesha idadi ya vifo kuongezeka Naibu Waziri Dkt. Ndugulile amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa na idara ya Afya mkoa wa Simiyu kuangalia chanzo cha ongezeko hilo na kuchukua hatua stahiki dhidi ya vifo hivyo ili kukomesha kabisa vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi.

Aidha, Dkt. Ndugulile ameuomba uongozi wa mkoa wa Simiyu kufuatilia watu zaidi ya 10000 walioonekana kuacha kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) ili kuweza kukabiliana na maambukizi mapya.

Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa viongozi na jamii mkoani Simiyu kuendelea kupambana na mimba za utotoni kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wote wa kike wanakwenda shule na kuwachukulia hatua kali wale watakaobainika kuwapa wanafunzi mimba kwani mimba za utotoni pia zimekuwa chanzo cha ongezeko la vifo vya akina mama wajawazito.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo imeendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanaume wanaobainika kuwapa mimba wanafunzi ambapo amebainisha kuwa hadi sasa ni takribani watu 9 wameshachukuliwa hatua.

Kuhusu suala la VVU Mhe. Mtaka amesema Serikali mkoani humo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwahimiza wananchi kupima VVU huku akibainisha kuwa idara ya afya itafanya mpango wa kuweka huduma za ushauri na kupima VVU pamoja na magonjwa yasiyoambukiza katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane kwa kuwa itahusisha watu kutoka maeneo mbalimbali.

Mhe. Dkt. Ndugulile akiwa wilaya ya Bariadi na Itilima ametembelea Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD)la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Jengo la Kituo cha Afya Ikindilo, Wodi ya Wazazi katika zahanati ya Nangale na Migato ambapo amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi iliyofanyika na thamani ya fedha iliyotumika

Akiwa katika wilaya ya Itilima ameahidi kulifanyia kazi ombi la Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi na Diwani wa Kata ya Migato Mhe. Mbuga Ntobi la kujenga kituo cha Afya katika Kata ya Migato kwa kulipeleka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ili wananchi waweze kusogezewa huduma jirani.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, mara baada ya kutembelea Jengo la Wagonjwa wa Nje la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wakati wa ziara yake mkoani humo Julai 22, 2018
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Mageda Kihulya (kushoto) akimuongoza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile(kulia) kuelekea katika wodi katika Hospitali Teule ya mkoa, wakati akiwa katika ziara yake mkoani humo, Julai 22, 2018.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile akiweka jiwe la msingi la Wodi ya wazazi katika Zahanati ya Migato Wilayani Itilima, wakati wa ziara yake wilayanihumo mkoani Simiyu, Julai 22, 2018.
Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga akisoma jiwe la msingi lililowekwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile( wapilikushoto) wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Itilima mkoani Simiyu, Julai 22, 2018.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile(kushoto), akiwaonesha Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Itilima, Mhe. Mahamoud Mabula nembo maalum zilizopo katika dawa zote za Serikali, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu,Julai 22, 2018.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile(kulia) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(katikati) na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa wakati wa ziara yake mkoani humo, Julai 22, 2018.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile(katikati) akitoka kuweka jiwe la msingi katika Wodi ya wazazi katika Zahanati za Migato wakati wa ziara yake mkoani humo, Julai 22, 2018
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akimjulia hali mgonjwa katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, wakati alipotembelea hospitali hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo, Julai 22, 2018.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile akiwaonesha wananchi wa Kata ya Ikindilo alama maalum inayotambulisa dawa za Serikali ambayo ni ‘msd GOT”, wakati akiwa kwenye ziara yake Mkoani Simiyu, Julai 22, 2018.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com