NAIBU WAZIRI WA AFYA ASIMAMISHA UJENZI WA JENGO LA UPASUAJI


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo juu ya ubora wa utoaji huduma za afya mbele ya watumishi wa Serikali.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile amesimamisha ujenzi wa jengo la upasuaji kutokana na kukosa misingi ya kitaalamu wakati wa ujenzi wa jengo hilo.

Waziri Ndugulile amesitisha ujenzi huo, akiwa katika ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma na ujenzi wa majengo ya kituo cha Afya cha Katoro mkoa wa Geita ambapo amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa wilaya Geita January Bikuba kuhakikisha anasimamia ufungaji wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato katika kituo hicho.

"Sasa jengo lile la upasuaji nimelisimamisha, Mganga Mkuu wa Mkoa, Mganga mkuu wa Wilaya mkae na wataalamu mfanye mapitio ya jengo hili, ili kabla ya jengo halijakamilika basi ushauri wa kitaalamu uzingatiwe, Thieta ni mahala patakatifu sana, ni lazima tuhakikishe kwamba misingi ya wataalamu wa Afya inazingatiwa",amesema Dkt Ndugulile.

Naye Katibu tawala wa mkoa wa Geita Selestine Gesimba amesema kuwa Mkoa wa Geita unasimamia huduma za afya kupitia vituo 171 vya kutolea huduma za Afya, ikiwepo hospitali 5 huku kati ya hizo tatu zikiwa chini ya Serikali, vituo vya Áfya 21 huku 17 vikiwa vinasimamiwa na Serikali.

Mbali na kuzuia ujenzi wa kituo hicho Waziri Ndugulile pia mnamo Julai 22, aligoma kuzindua majengo ya chuo cha Afya cha waganga wasaidizi mkoani Mara kutokana na kutoridhishwa na matumizi ya fedha ya kiasi cha shilingi milion 500 kilichotolewa kwa ajili ya ujenzi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post