MWENYEKITI ATUMIA FEDHA ZA KIJIJI KUMTIBU MKEWE


Wakazi wa kijiji cha Buhororo wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wamemweka kiti moto mwenyekiti wao, Stanford Simon wakimtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma za kutafuna Sh477,000 zilizochangwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.


Hata hivyo, Simon alijitetea kuwa alitumia fedha hizo kugharamia matibabu ya mkewe kutokana na dharura ya ugonjwa uliotokea, hivyo kuomba kuzirejesha kwa awamu ndani ya miezi mitatu.


“Kibinadamu nisingemwacha mke wangu apoteze maisha kwa kukosa fedha za kugharamia matibabu yake huku ninazo fedha za kijiji.


“Nililazimika kuchukua uamuzi mgumu wa kujikopesha na kumpeleka hospitali kuokoa maisha yake, naahidi kurejesha hadi senti ya mwisho,” alisema.


Naye mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza ukweli wa jambo hilo na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.


Awali, hoja hiyo iliibuka wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kijijini hapo, mwenyekiti huyo alidaiwa kutafuta michango ya wakazi 46 wanaonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).


Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha ya serikali ya kijiji hicho, Emily Simon alisema baada ya kupokea fedha hizo, mwenyekiti wake alizitumia bila ridhaa ya wajumbe wa serikali ya kijiji.


Alisema kutokana na kutafunwa kwa michango hiyo ujenzi wa zahanati ya kijiji umekwama.


Baada ya kuwapo kwa tuhuma hizo, zaidi ya wananchi 4,000 kutoka kaya 874 waligoma kuendelea kuchanga Sh30,000 kila mmoja kwa hiari zilizopitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.


“Hadi michango inakwama, zaidi ya Sh3.7 milioni zilikuwa zimekusanywa na kufanikisha ujenzi kuanza kwa ngazi ya msingi kabla ya kusimama kutokana na kukosekana kwa fedha za kuwalipa mafundi,” alisema Simon.


Kiongozi wa mafundi waliojenga msingi wa zahanati hiyo hiyo, Richard Mwita alisema vibarua wanadai zaidi ya Sh1.7 milioni hivyo wamefikia uamuzi wa kutoendelea na kazi kushinikiza walipwe.


Mmoja wa wanufaika wa mpango wa Tasaf, Mariam James alisema alichanga Sh20,000 bila kupewa stakabadhi ya malipo.

Na Shaaban Ndyamukama, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post