MKUU wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (pichani) amezindua rasmi kampeni ya upimaji virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU 'ARVs' mapema kwa wanaume ikiwa na ujumbe wa “Furaha yangu, Pima, Jitambue, Ishi.”
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika Julai 28,2018 katika kata ya Tinde wilayani Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi wa kiserikali kutoka wilaya zote za mkoa wa Shinyanga na wageni mbalimbali akiwemo balozi wa kampeni hiyo, msanii Joy Makini.
Katika hotuba yake kwa wananchi mkuu wa mkoa Zainab Telack amewaomba wakazi wa mkoa wa Shinyanga hususani walengwa wa kampeni hiyo wanaume kujitokeza kwa wingi ili kupima afya zao na watakaobainika kuambukizwa waanze kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU 'ARVs'.
“Lengo la kampeni hii ni kuhamasisha jamii, hususan wanaume kupata huduma za unasihi, upimaji na uanzishaji wa dawa mapema, tupo hapa leo ili kukumbushana kwamba kila mtu ana wajibu wa kupima, niwaombe akina baba wote tushiriki kikamilifu kwenye kupima afya zetu.”
Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wale wote watakaojitambua kwamba wameathirika, waanze kutumia dawa mapema ili waweze kuishi kwa furaha na kwamba kuwa na virusi vya UKIMWI siyo mwisho wa mtu kuishi.
Kwa upande mwingine mkuu huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto kuzungumza na watoto wao bila kuona aibu kuhusu suala zima la malezi yao na wajiepushe na mahusiano ya kimapenzi yanayosababisha kujiingiza kwenye vitendo vya ngono.
“Ni muhimu wazazi na walezi sasa mchunge watoto wenu, angalieni mahusiano ya watoto awe wa kike au wa kiume, msiseme tu eti atapata mimba, hujui atapata mimba peke yake ataweza kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI,”
“Ni kijana unaona anahangaika na kila mwanamke, zungumzeni nao ili tupunguze maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI ambayo hayana sababu, na hili tukiamua sote kwa pamoja inawezekana,” alieleza Telack.
Katika taarifa yake mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Rashidi Mfaume alisema hali ya maambukizi ya UKIMWI kwa mkoa wa Shinyanga hivi sasa inaonesha kushuka kutoka asilimia 7.4 mwaka 2011/2012 na kufikia asilimia 5.9 kwa takwimu za mwaka 2016.
Hata hivyo alisema kiwango cha sasa bado kipo juu ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia ambapo amesema pamoja na uhimizaji wa wananchi kujitokeza kupima afya zao kwa hiari lakini bado wengi wao hawajaitikia wito huo.
“Mkoa wetu unatajwa kuwa na watu 68,572 wanaoishi na maambukizi ya VVU, hadi Desemba, 2017 lakini hadi kufikia Juni, 2018 53,445 sawasawa na asilimia 88 tayari walikuwa wameanza huduma za tiba na matunzo,”
“Wapo watu wana maambukizi lakini hawafahamu afya zao, wanaishi na VVU, inakadiriwa kwamba takribani 15,127 sawa na asilimia 22 bado hawajatambua hali zao za maambukizi, huu ni wastani, na hawa watu wapo kati yetu, kwamba kuna watu miongoni mwetu katika hadhara hii wana VVU lakini hawafahamu hali zao, na lengo la kampeni hii ni kwa wale ambao wameambukizwa lakini hawafahamu hali zao za maambukizi,” alieleza Dkt. Mfaume.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Mshauri wa mradi wa tohara kwa wanaume mkoani Shinyanga, Dkt. Innocent Mbughi kutoka Shirika la Intra health alisema kampeni ya tohara kwa wanaume imeonesha mafanikio kutokana na wananchi wengi kujitokeza kufanyiwa tohara.
Dkt. Mbughi alisema tohara kwa wanaume inasaidia sana watu kutoambukizwa virusi vinavyosababisha UKIMWI kwa asilimia 60 kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika hapa nchini na kwamba kiwango cha maambukizi kwa mkoa wa Shinyanga kimeshuka hivi sasa.
“Tohara kwa wanaume ina asilimia 60 ya kumkinga mwanamume dhidi ya maambukizi ya UKIMWI na mbali ya faida hizo, lakini pia tohara inamsaidia mwanamume asiweze kupata magonjwa ya ngono ikiwemo kaswende lakini pia ni usafi,”
“Lakini mbali ya hayo, tohara kwa mwanamume inamsaidia asipate saratani ya uume, pia inamsaidia mwenza wake yaani mwanamke asiweze kupata kansa ya mlango wa kizazi kirahisi,” alieleza Dkt. Mbughi.
Dkt. Mbughi alisema hadi kufikia mwezi Juni, 2018 wanaume waliofanyiwa tohara ni 48,000 zaidi ya asilimia 88 ya lengo la kufikia watu 54,800 na kwamba changamoto kubwa ni vijana wengi kutojitokeza kufanyiwa tohara.
Uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya msingi Tinde wilayani Shinyanga ulienda sambamba na maonesho ya mabanda mbalimbali na utolewaji wa upimaji wa hiari wa virusi vya UKIMWI ikiwemo kutahiri kwa wanaume.
Na Suleiman Abeid - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza wakati wa uzinduzi wakampeni ya upimaji virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia ARV mapema kwa wanaume ikiwa na ujumbe wa “Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi.”. Picha zote na Suleiman Abeid Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upimaji virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia ARV mapema kwa wanaume
Msanii Joy Makini akihamasisha wanaume kupima VVU
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza wakati wa uzinduzi wakampeni ya upimaji virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia ARV mapema kwa wanaume ikiwa na ujumbe wa “Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi.”. Picha zote na Suleiman Abeid Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upimaji virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia ARV mapema kwa wanaume
Msanii Joy Makini akihamasisha wanaume kupima VVU
Social Plugin