Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack ameendesha harambee (fund rising) ya ulipaji fidia wa eneo la ekari 18 na ujenzi wa kituo cha polisi wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Harambee hiyo kwa ajili ya ununuzi wa eneo na ujenzi wa kituo cha polisi cha wilaya ya Kishapu imefanyika jana Julai 20,2018 katika ukumbi wa shule ya sekondari Kishapu.
Katika harambee hiyo iliyoshirikisha wadau mbalimbali jumla ya fedha zote zilizotolewa pamoja na ahadi ni Tsh.49,920,000/=.
Mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack alisema ujenzi huo unatarajiwa kuanza haraka iwezekanavyo mara tu ramani ya kituo hicho itakapopatikana.
Michango iliyochangwa papo hapo wakati wa harambee hiyo ni shilingi 1,840,000/=,hadi shilingi 48,080,000/=,ahadi za vifaa vya ujenzi mifuko ya saruji 156.
Aidha mgodi wa almasi wa Mwadui Williamson Diamonds Ltd uliahidi kuchangia mabati yote ya kuezekea na saruji ya kutosha muda wote wa ujenzi huku Jeshi la Magereza Shinyanga likiahidi kutoa nguvu kazi kwa ajili ya ujenzi huo.
Miongoni mwa wadau walioshiriki harambee hiyo ni Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Shinyanga,Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya kishapu,Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya ya Kishapu wawakilishi kutoka migodi ya Almas ya Williamson Diamonds LTD na El Hilal,uongozi wa Benki ya NMB tawi ka Kishapu wafanyabiashara na wananchi wa kawaida.