Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROGRAMU YA 'UNI LIFE CAMPUS' YAFANIKISHA NDOTO ZA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU TANZANIA


Mwanzilishi wa programu ya 'Uni Life Campus' Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Esther Mmasi ambaye anawakilisha Vyuo Vikuu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na wanafunzi wa vyuo mbali mbali vya Tanzania wakati wa semina elekezi juu ya kuzitunza fursa wanazozipata katika maisha yao ikiwa ni pamoja na kupatiwa nafasi za kufanya mafunzo kwa vitendo (field) katika taasisi mbali mbali za serikali na mashirika binafsi mwishoni mwa wiki iliyopita katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam. Picha zote na Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Mkurugenzi DM Saikolojia Limited Bw. Dosi Said Dosi akitoa neno kwa wanafunzi wanaotarajia kuanza mafunzo yao kwa vitendo (field) wakati wa semina elekezi juu ya kuzitunza fursa wanazozipata katika maisha yao katika taasisi mbali mbali za serikali na mashirika binafsi mwishoni mwa wiki iliyopita katika Chuo cha CBE jijini Dar es Salaam.
Meza kuu wakifuatilia kwa makini.

Mmoja ya maofisa katika Programu ya 'Uni Life Campus' Gladness akitoa maelezo machache kwa wanafunzi.
Rais wa Wanafunzi, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Said Hamisi Suba akitoa shukrani zake.
Mratibu wa Programu ya 'Uni Life Campus' Elibariki Abel akitoa muongozo wa masuala mbalimbali kwa wanafunzi.
Mwanafunzi Agustino wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) akiuliza swali.
Mwanafunzi Abdulatif wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam akiuliza swali.

Mhe. Esther Mmasi (katikati mwenye miwani) akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa vyuo mbali mbali waliohudhuria katika semina elekezi mara baada ya kupatiwa nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field) katika taasisi mbali mbali za serikali na mashirika binafsi mwishoni mwa wiki iliyopita Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania waaswa kuzilinda na kuzitunza fursa wanazozipata ili ziweze kuwaletea maendeleo endelevu katika maisha yao.

Hayo yamesemwa na Mwanzilishi wa programu ya 'Uni Life Campus' Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Esther Mmasi ambaye anawakilisha Vyuo Vikuu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita katika semina elekezi ya kuwaasa wanafunzi waliopata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field) katika tasisi mbali mbali za serikali na mashirika binafsi.

"Nawaomba sana wanavyuo wenzangu huko mnapokwenda mkawe mabalozi wema, mzingatie kuwa watiifu na muwe na moyo wa kujifunza huku mkifanya kazi kwa bidii hapo mnaweza kupata maarifa mapya," amesema Mhe. Esther Mmasi.

Amesema kuwa tatizo la vijana wengi kwa sasa wamekuwa ni wakaidi na wanaoendeleza uvivu huku simu ikiwa ni kikwazo kikubwa pindi wanapofanya kazi.

"Mkienda kwenye mafunzo kwa vitendo (field) mzingatie kufanya kazi na si kushinda unachezea simu maana wengi wenu kutwa kucha ni kuchat tu unasahau hata kilichowapeleka katika ofisi za watu, nangoja ripoti njema zitakazowajenga mbeleni",amesema.

Aidha amesema kuwa mpka sasa Programu ya 'Uni Life Campus' imewatafutia nafasi za mafunzo kwa vitendo (field) wanafunzi wapatao 100 waliokuwa wameomba kutoka vyuo mbali mbali Tanzania na watakwenda Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Benki ya NMB na Benki ya Posta Tanzania (TPB).

"Tunamshukuru Mungu tumeweza kuwatolea changamoto wanafunzi hasa waliokuwa wakiomba mafunzo kwa vitendo, tulipotangaza mwaka jana mwishoni zaidi ya vijana 1,900 waliweza kuomba ila tumeweza wapatia nafasi 100 ambao tulizipata licha ya kuendelea kuongea na taasisi mbali mbali za serikali ambazo zimetuahidi kutupatia nafasi zaidi ya 600," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi DM Saikolojia Limited Bw. Dosi Said Dosi aliwaasa wanafunzi hao kufuata kile kitakachokuwa kimewapeleka na kuacha kujirahisisha na kujikuta wakitumika.

"Unajua unaweza kwenda kwenye maofisi lakini kama hautakuwa na msimamo utaishia kuwa mpira wa kona ambao kila mtu anaweza kupiga na kufunga goli, niwaombe sana mkawe mabalozi wema wa programu ya 'Uni Life Campus' ili mrudi na matokeo chanya yatakayowaweshesha mbeleni kupata kazi kwa urahisi. Kumbukeni huko mnaenda kufungua milango yenu ya mafanikio," amesema Bw. Dosi.

Nae mwanafunzi Agustino wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) aliyepatiwa nafasi ya kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo alimshukuru Mhe. Esther Mmasi kwa kuweza kupata maono ya kuanzisha programu ya 'Uni Life Campus' ambayo imekuwa chachu ya kuwafungulia milango ya kupata mafunzo kwa vitendo bila ya kupiga hoi mlango kwa mlango katika makampuni.

"Binafsi nilikuwa siamini programu ya 'Uni Life Campus' kama inaweza kufanikisha hiki ilichokifanya leo maana jambo ambalo limekuwa ni msalaba kwa wanafunzi wengi ni suala la uataji wa nafasi za kufanya kazi kwa vitendo (field), ila kwa sasa limefanikishwa kilahisi sana, niwashukuru sana kwa moyo wao huo maana tumeweza kupata bila hata ya kutoa hela yeyote," amesema Mwanafunzi Agustino.

Programu ya 'Uni Life Campus' imeanzishwa ili kuweza kuwaongezea wanafunzi wa Vyuo Vikuu kiwango cha kujitambua kwa wanafunzi ili kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa vyuoni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com