Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua juzi Ikulu jijini hapa, Rais Magufuli alichambua sababu za kufanya mabadiliko katika wizara hiyo alipokuwa akizungumzia matarajio yake kwa Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola ambaye amechukua nafasi ya Dk Nchemba pamoja na katibu mkuu mpya na naibu katibu mkuu wa wizara hiyo.
Baadhi ya sababu hizo ni jinsi alivyoshindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu kushughulikia suala la kufunga mashine za alama za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (AFIS) katika vituo 108 vya polisi uliofanywa na kampuni ya Lugumi kwa gharama ya bilioni 37.
Nyingine ni mkataba wa ununuzi wa magari 777 ya polisi, kushughulikia changamoto zinazolikabili Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ajali barabarani, usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), kupandishwa vyeo kwa askari, masuala ya wakimbizi na kuhakikisha wafungwa wanazalisha mali. “Ukiondoa kazi zinazofanywa na makamishna wahusika wenyewe kwa kila mmoja na eneo, sijapendezwa na uongozi wa juu. Nakupeleka pale (Lugola) ukafanye kazi na wewe bahati nzuri ni askari,” alisema.
Mambo 13
Akizungumzia suala la Lugumi Rais Magufuli alisema, “Nilifanya uchunguzi wa mradi wa polisi, vituo 108 ambapo palikuwa na mkataba wa Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na mtu anaitwa Lugumi wa Sh37 bilioni tulipewa maagizo na Bunge kama Serikali tuyashughulikie na tuyatafutie ufumbuzi lakini mpaka leo hii haijapatiwa ufumbuzi.”
Jambo jingine ni mkataba wa kuagiza magari 777 ya polisi ambao Rais Magufuli alisema ulikuwa wa ovyo. “Nazungumza ili Watanzania wote wajue, magari ambayo yameanza kuletwa kwenye mkataba huo yameandikwa kuwa ni mapya lakini yalishaanza kutembea zaidi ya kilomita 4,000.”
Pia alisema bei za magari hayo zilikuwa za ovyo na kumuagiza Lugola na viongozi wengine wa wizara hiyo, “Mkaupitie huo mkataba huo.”
Aligusia pia suala la ununuzi wa sare za polisi ambao uligharimu mamilioni ya fedha lakini hazikuonekana na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
“Ndio maana nayazungumza hapa hadharani kwa sababu sijapata majibu sahihi. Niliowapeleka pale hawakutatua matatizo haya, zilisambazwa sare za polisi kwa mabilioni ya fedha hazionekani nataka haya ukayashughulikie,” alisema.
Alisema kuna fedha za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) zilitumika vibaya, viliagizwa vifaa ambavyo vingine havikufika. Alisema walichukua hatua ya kuwasimamisha kazi waliohusika lakini waliofanya mambo hayo hawajachukuliwa hatua zozote.
“Kuna mambo yanafichwafichwa, pana delaying technic. Mambo yote yanajulikana. PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Takukuru) napo naona wanapachezea kwelikweli… hilo nalo ukaliangalie,” alisema Rais Magufuli akiendelea kuchambua uozo wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Sababu nyingine aliyoitaja Amiri Jeshi Mkuu ni jinsi waziri huyo wa zamani alivyoshindwa kusimamia masilahi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, “Kuna masuala mengine, ukayaangalie kwenye vyombo unavyoviongoza. Kwa mfano, Zimamoto kuna magari 53 pekee nchi nzima na magari haya ni ya zamani, hatujawahi kuletewa taarifa kuwa kuna shida tunasikia sikia tu, lakini kwenye sherehe wanahudhuria, sasa ukasimamie tuwe na vifaa ambavyo vitasaidia kutatua majanga ya moto.
Kingine kilichomng’oa Dk Nchemba Mambo ya Ndani ni mfululizo wa ajali za barabarani bila hatua kuchukuliwa. “Nimechoka kutuma rambirambi, kila siku inatoka (ajali) hii inakuja hii na kwa bahati mbaya ni mimi pekee ndiye ninayetuma rambirambi. Waziri wa Mambo ya Ndani hahangaiki kutuma rambirambi. Ninasema nimechoka kutuma rambirambi. Kwa mfano, Mbeya katika wiki mbili yamefululiza matukio mawili, hakuna hatua ya kuchukua hata ya kumwambia RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) au RTO (Kamanda wa Polisi Usalama Barabarani wa Mkoa) ajiuzulu. Wameshakufa 40 mnataka wafe wangapi ndio RPC ajiuzulu? Si umpunguzie nyota ili ajue uchungu wa damu zilizomwagika pale. Hiyo kazi siyo ya Rais ni ya waziri tu hata katibu mkuu, wewe mkoa wako kila siku ni ajali na unaitwa RPC. Sasa ukaanze na PRC wa Mbeya na RTO.
Rais pia alizungumzia dosari zilizopo katika uandikishaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) katika wizara hiyo. Alisema wizara nyingi zinafanya mambo ya ovyo na kumtaka waziri huyo akachambue na kubaki na NGO zinazoshughulika na masuala yenye masilahi na Watanzania.
Kupandishwa vyeo kwa askari hasa wa ngazi za chini ni jambo jingine lililomng’oa Dk Nchemba Mambo ya Ndani. Rais Magufuli alisema inashangaza kuona askari anafanya kazi akiwa na cheo cha chini kabisa kwa miaka 17 bila ya kupandishwa cheo chochote wakati hajahukumiwa wala kufanya kosa lolote.
Kingine ni utoaji holela wa vibali vya kazi akisema vinatolewa na kama njugu. Alimtaka Waziri Lugola akashughulikie suala hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi kwa kuwa mtu hawezi kupata kibali cha kazi kama hajapitia Uhamiaji.
Sasa hivi kuna kesi ya watu wameshikwa pale Oysterbay walikuwa wanatoa working permit (vibali vya kazi) wao wenyewe na wana mitambo yao ilibidi mimi mwenyewe nitoe taarifa polisi na mmoja wa watuhumiwa ni ofisa Uhamiaji, alitoka Rukwa.
Kuhusu wakimbizi, Rais Magufuli alisema, “Mlifuatilie, wakimbizi imekuwa mtaji kwa wale wanaofanya kazi kambi za wakimbizi. Mfuatilie mjue kama wanafanya kazi vizuri au wanatumika.”
Alizungumzia pia suala la wafungwa ambalo alishawahi kulitolea maagizo akitaka wafanye kazi za kuzalisha mali kama ilivyo kwa nchi nyingine. Alisema Tanzania inapata hasara ya kuwalisha, “Watumieni kuzalisha, ikiwezekana wafanye kazi mchana na usiku. Watumieni wafanye kazi kwelikweli ili wasirudie makosa.”
Alitaka hata waliopewa adhabu ya kifo nao wafanye kazi na kwamba kama kuna sheria inayozuia ifanyiwe marekebisho kama zinazofanyiwa nyingine.
“Nimezungumza sana kwa sababu wizara hii unaweza ukashinda kutwa unaizungumzia. Ina changamoto nyingi mno inaongoza kwa madai ya ovyo yaliyopelekwa Wizara ya Fedha, hivyo mfanye uhakiki wa madai mnayoyaomba.”
Lugola afunguka
Mara baada ya kuapishwa, Lugola alisema anaanza kuzifanyia kazi changamoto zilizobainishwa na Rais Magufuli mara moja kwa kuitisha kikao cha wakuu wa taasisi zote zilizo chini ya wizara.
“Nitakapofika ofisini nikajipanga na wenzangu, hapo tutakuwa na mikakati mingi zaidi. Nimepokea maelekezo ya Rais, nitakwenda kuyafanyia kazi,” alisema Lugola.
Waziri huyo mpya alisema anakwenda kuanza na suala la ajali za barabarani kama kipaumbele chake ili kuhakikisha zinapungua na wananchi wanakuwa salama kwenye safari zao.
Pia, alisema atahakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuwapo ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku na kujenga uchumi wa taifa.
Profesa Mbarawa na Kamwelwe
Mbali ya kuzungumzia udhaifu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Rais Magufuli alibainisha matarajio yake kwa waziri mpya wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa akimtaka kushirikiana na Katibu Mkuu wake, Profesa Kitila Mkumbo kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maji.
Aidha, alimtaka waziri mpya wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kuhakikisha miradi yote ya ujenzi wa barabara unakamilika kwa wakati hasa ikizingatiwa kwamba anaifahamu fika kazi hiyo. Akizungumza baada ya hafla ya kuapishwa, Profesa Mbarawa alisema anatambua changamoto za maji hapa nchini, hivyo atakwenda kuhakikisha miradi yake inatekelezwa kikamilifu na wananchi hasa wa vijijini wanapata majisafi.
“Makandarasi wajipange kufanya kazi kwa uadilifu, lazima value for money (thamani ya fedha) iwepo. Jukumu langu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji.”
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo alisema atasimamia suala la bei ya mazao ya kilimo na matumizi ya zana bora za kilimo katika uzalishaji.
Na Peter Elias na Asna Kaniki, Mwananchi
Social Plugin