Rais John Magufuli amesema amechoka kutuma rambirambi kufuatia wingi wa ajali za barabarani zinazopoteza maisha ya wananchi wengi.
Akizungumza leo Julai 2,2018 baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua Julai 1, Rais Magufuli amesema kuwa anashangazwa na kuwa yeye tu ndiye hutoa salamu hizo wakati Waziri wa Mambo ya Ndani yupo na anaenda kwenye mambo yake.
“Ajali za barabarani nimechoka kutuma rambirambi, unatuma hujakaa hata wiki unatuma tena, kinachosikitisha Waziri hatumi hata rambirambi wala haendi kuzika, unasikia tu yuko huko..! Hakuna hatua zinazochukuliwa” Rais Magufuli
“Kinachonisikitisha waziri na katibu makuu wao hawatumi hata rambirambi. Mfano mzuri ni ajali ya Mbeya watu 40 wamekufa hakuna hatua hata ya kuwaambia RPC na RTO wajiuzulu ili wajue uchungu wa damu zilizomwagika. Hiyo kazi si ya Rais ni ya waziri na hata katibu mkuu,” alisema Rais Magufuli.
Ameonesha pia kusikitishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kushindwa kuchukua hatua kwa watu waliotajwa kuhusika na ufisadi kupitia mradi wa vitambulisho vya taifa na mingineyo.
“Kuna pesa za Nida zilichezewa ovyo ovyo tukachukua hatua kuwasimamisha wahusika lakini waliofanya hivyo sijaona hatua zilizochukuliwa kwa waliofanya ovyo. Je, pesa wamerudisha? Alihoji Rais Magufuli na kuongeza kuwa kuna ucheleweshaji wa kutoa maamuzi katika suala hilo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemtaka waziri mpya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kusimamia vitengo vyote vya wizara yake na akieleza wazi wazi kusikitishwa na kutojaliwa kwa idara ya Zimamoto.
“Wizara ina mambo mengi na vitengo vyake, Zimamoto wana magari 53 tu lakini sikumbuki kuletewa maombi ya Zimamoto. Haya tumeyajua kwa kuuliza uliza tu lakini wenye wizara hawasemi,” aliongeza.