Nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo
Tetesi za nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo kutakiwa na klabu ya Juventus zimepelekea hisa za klabu hiyo ya Italia kupanda katika kipindi cha siku chache za karibuni huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa staa huyo kutua katika klabu hiyo.
Muda mfupi baada ya tetesi hizo kusambaa mitandaoni mapema Jumatano, Juventus ilipanda kwa asilimia 5.89 katika soko la hisa huku kukiwa na ongezeko la asilimia 3.2 katika siku hiyo moja.
Inaelezwa kuwa Juventus imepeleka ofa ya Pauni 88 millioni kwa Real Madrid kwaajili ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo mwenye miaka 33 ambaye anaonekana kutokuwa na furaha na namna anavyolipwa katika klabu yake, akitaka kulipwa sawa na Messi.
Messi alisaini mkataba mpya mwezi Novemba mwaka jana wa kuendelea kuitumikia klabu ya Barcelona ambao unamfanya sasa kulipwa Pauni 500,000 kwa wiki huku Ronaldo alilipwa Pauni 365,000 katika mkataba wake wa sasa ambao alisaini mwaka 2016.
Kwa sasa Ronaldo yuko likizo baada ya timu yake ya taifa ya Ureno kuondolewa katika hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la Dunia dhidi ya Uruguay kwa kufungwa 2-1 .
Baada ya fainali ya Uefa Champions League , Ronaldo aliahidi angezungumzia mustakabali wake katika kambi ya timu ya taifa lakini hakufanya hivyo huku taarifa nyingi zikidai kuwa huenda Juventus wakafankisha usajili huo.