Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imewataka wataalam wa afya 6,180 walioajiriwa kuripoti katika vituo vyao ya kazi ndani ya siku 14.
Wataalam hao wa afya watasambazwa katika vituo vya afya, hospitali za Wilaya na zahanati nchini.
Akizungumza leo Juni 9, 2019 na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo amesema atakayeshindwa kuripoti ndani ya muda huo, ajira yake atapewa mwingine.
Mei 10, 2018 Jafo alitangaza nafasi za ajira hizo na kubainisha kuwa watumishi watakaoajiriwa watapangiwa kwa kuzingatia mahitaji, kuwataka wenye sifa za taaluma katika kada ya afya wajitokeze kuomba nafasi kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi.
“Wasijikusanye katika ofisi za mjini kwasababu hatutabadilishia vituo kwa kuwa walipoomba ajira walisema wapo tayari kufanya mahali popote ndani ya Tanzania," amesema Jafo leo.
Jafo amesema upangaji wa watumishi hao umezingatia halmashauri ambazo zina zahanati na vituo vya afya lakini hazina watumishi, vituo vya afya 210 ambavyo vilikarabatiwa na zahanati ambazo zilikuwa zinaongozwa na wahudumu wa afya.
Ametaka wananchi kuwapokea wahudumu wa afya ili wawatumikie na waache kuwafanyia mambo mabaya kama katika baadhi ya maeneo ilivyokuwa ikifanyika.
Amesema majina ya walioajiriwa yanapatikana katika tovuti ya Tamisemi.
Social Plugin