Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SUMAYE ASIKITISHWA NJAMA ZA KUFUTA UPINZANI TANZANIA

Waziri Mkuu mstaafu, Fedrick Sumaye, ameweka kile alichokieleza njama za kufuta upinzani nchini na kutahadharisha kuwa kufanya hivyo ni kuondoa sauti, uhuru wa watu na kwamba jambo hilo ni hatari kwa mustakabali wa taifa.


Sumaye ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, alieleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa marudio wa udiwani Kata ya Makorola jijini Tanga.


Alisema kufuta upinzani ni kukataa demokrasia, hivyo kuwafanya watu wakose mahali pa kusemea kero zao, jambo alilolifananisha na bomu ambalo alidai linaweza kuleta madhara makubwa litakapo kuja kulipuka.


Aliwataka Watanzania watambue kuwa kufutika upinzani nchini ni kusababisha mapambano na kuondoa amani iliyopo kwa kuwa kushindana kwa vyama ndiyo nguzo ya amani.


“Watanzania msishabikie kuua upinzani maana yake mnashabikia kuua demokrasia na kuondoa sauti za watu, maendeleo na uhuru wa watu kuongea matatizo yao,” alisema Sumaye.


Alisema sababu ya kufanyika chaguzi ndogo kila mara ni dalili za kukosekana kwa demokrasia ya kweli na kwamba mabilioni ya fedha yanayotumika kwenye uchaguzi huo yangetumika kuondoa kero mbalimbali za kijamii.


Alieleza athari nyingine ya kuua upinzani ni kuzalisha vibaraka wengi na kudumaza maendeleo na kuvishauri vyombo vya dola kutoingilia masuala ya uchaguzi huo badala yake kazi hiyo iachwe kwenye ushindani wa vyama vya siasa.


Alimwombea kura mgombea wa kata hiyo anayeungwa mkono na Ukawa, Zainab Ashiraf, ambaye alisema kumchagua kuwa diwani pamoja na mambo mengine, ni kukataa ukandamizwaji wa demokrasia nchini.


Mkutano huo uliofunguliwa na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Wilaya ya Tanga, Richard Abel, ulihudhuriwa na vyama vinavyounda Ukawa ambao ni mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe na Jonatha Bahweje ambaye ni katibu wa Chadema Mkoa Tanga.


Wengine waliohudhuria na kupewa nafasi ya kuzungumza ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF, Amour Abal-hasan; Kamishna wa NCCR- Mageuzi, Ramadhan Manyeko na Mbunge Viti Maalum Chadema, Yosephar Komba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com