Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TARATIBU ZA KUAGWA ,MAZISHI YA MBUNGE MAJI MAREFU....MWIGULU,UMMY, NAPE WAIBUKA


Aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu enzi za Uhai wake.


Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu, utaagwa kesho Julai 4,2018 na baadaye mwili kusafirishwa kuelekea jimboni kwake Korogwe kwa ajili ya maziko Julai 5,2018.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Hillary Ngonyani ambaye ni Msemaji wa Familia (kaka wa marehemu) kesho Julai 4,2018 mwili utaagwa kwenye viwanja vya Bunge la kwanza la Tanganyika, Karimjee kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kabla ya kuanza safari ya kwenda Korogwe kwa mazishi. 

Amesema msiba utakuwa nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Masuguru mjini Korogwe maarufu kama Mamba Club.

"Mazishi yatakuwa Julai 5, 2018 siku ya alhamisi saa 10 jioni kwenye makaburi ya kijiji cha Kwamndolwa. Ni baada ya kuswaliwa saa saba mchana kwenye Msikiti Mkuu wa Ijumaa mjini Korogwe" alisema Ngonyani.

"Majimarefu amefariki dunia Juni 2, 2018 saa tatu usiku kwenye chumba namba moja cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Muhimbili, na alikuwa anasumbuliwa na Homa ya Mapafu kwa muda mrefu",amesema.

"Pamoja na kuumwa arnimonia kali (homa ya mapafu), mara chache alikuwa anasumbuliwa na presha ya kushuka. Kabla ya hapo alikuwa anasumbuliwa na nyonga, na hiyo ilimfanya alazwe nchini India mwezi mmoja", amesema Ngonyani ambaye yeye ndiyo aliyemlea Majimarefu.

Ngonyani amesema, Maji Marefu ameacha wake wawili Salma na Halia. Ni baada ya hivi karibuni kufiwa na mke mkubwa Bi. Mariam, huku watoto wakiwa 11, watoto wa kike sita na kiume watano.


Na kati ya watoto hao wa kiume, mmoja ana siku tano tangu kuzaliwa kwake, na amepewa jina la Hillary ambaye ni baba yake mkubwa.

June 6, 2018 mbunge huyo alifiwa na mkewe, Mariam aliyekuwa akipatiwa matibabu hospitali ya taifa pia.
Kifo cha  Prof. Maji Marefu kimeibua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba na kuunga na viongozi wengine wa CCM katika kutoa salamu za pole.

Dkt. Mwigulu ambaye amevuliwa nyadhfa zake na Rais Magufuli mwishoni mwa wiki iliyoisha kupitia mtandao wake wa kijamii amesema kwamba CCM imepata pigo kubwa kwa kumpoteza kada na kiongozi wa kweli.

"Maandiko matakatifu yanasema, mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi si nyingi. Tumempoteza kaka, ndugu na rafiki comrade Stephen Hilary Ngonyani(Prof. Maji Marefu), tumempoteza kiongozi na kada kweli kweli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)", ameandika Mwigulu.

Mbali na Mwigulu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa pole zake kwa familia huku akiwataka wawe na ustamilivu katika kipindi hiki kigumu walichokuwa nacho.

"Mbele yako, nyuma yetu. Pumzika kwa amani kaka yetu Stephen Ngonyani (Prof. Maji Marefu). Natoa pole nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi wa Korogwe Vijijiji. Mwenyezi Mungu awape ustamilivu katika kipindi hiki kigumu", ameandika Ummy.

Pamoja na hao pia Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye ameguswa na kifo hicho cha kada mwenzao wa CCM na kumuombe dua marehemu huko aendapo.

"Kaka na rafiki wa kweli, pumzika kaka", ameandika Nape.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com