SHIRIKA lisilo la kiserikali la Twaweza, limejibu barua ya
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech),
iliyowataka kueleza taratibu walizotumia wakati wa
kufanya utafiti wa umaarufu wa viongozi wa kisiasa
nchini.
Akizunguma jana na Nipashe kwa njia ya simu, Ofisa Mawasiliano wa Twaweza, Annastazia Rugaba,
alisema walijibu barua hiyo tangu Ijumaa iliyopita.
“Hatuwezi kueleza tulichowajibu kwa kuwa yalikuwa ni mawasiliano kati ya taasisi na taasisi, ila
tumeshawajibu kabla ya muda wa siku saba waliotupa,” alifafanua baada ya kutakiwa kueleza
majibu yao.
Nipashe iliwasiliana na Costech kutaka kujua ni lini uamuzi kuhusu shauri hilo utatolewa baada ya
Twaweza kujieleza kutokana na kushindwa kufuata taratibu wakati wa kufanya utafiti wa umaarufu
wa viongozi wa kisiasa, Kaimu Mkurugenzi wa Costech, Dk. Amos Nungu, alisema maamuzi yoyote
yatakayotolewa dhidi Twaweza, hayatakuwa hadharani kwa kuwa yalikuwa mawasiliano ya ndani.
“Hatutarajii kutoa chochote kitakachojadiliwa nje kwa sababu siyo nia yetu, ilikuwa bahati mbaya
kwamba ile barua ilikwenda kwenye mitandao, hivyo hata majibu yatakuwa ndani ya taasisi na
taasisi,” alifafanua.
Aidha, alisema majibu ya barua kutoka Twaweza yalishapokelewa na yanafanyiwa kazi na Costech.
Wiki iliyopita, mkurugenzi huyo alisema “Tume inayo kamati maalum inayohusika na kusajili na
kutoa vibali kwa tafiti mbalimbali zinazoendeshwa Tanzania.
Maombi hupelekwa kwa wataalamu
waliobobea katika nyanja husika kabla ya kuletwa kwenye kamati ili kujadiliwa.
Alisema Tume imekuwa ikiwasiliana na wadau pale wanapobaini utafiti kufanyika bila kusajiliwa ama
kufuata taratibu na ndiyo maana iliwasiliana na Twaweza.
Dk. Nungu alisema siyo mara ya kwanza Costech kuwaandikia barua wadau wake na Twaweza siyo
wa kwanza kuandikiwa barua ya namna hiyo.