Mabao ya wachezaji wa akiba wa Ubelgiji Marouane Fellaini Nacer Chadli walioingia dakika ya 65 yamegeuza mchuano wa kukata na shoka ugani Roistov Arena na kuifikisha Ubelgiji robo fainali.
Red Devils watacheza robo fainali kwa mara ya tatu kwenye historia yao baada ya kufuzu 1986 na 2014.
Ubelgiji ilihangaishwa mapema kupitia magoli ya Haraguchi dakika ya (48) na Inui kunako dakika ya (52) lakini mabadiliko ya kocha Roberto Martinez yalipindua mchezo.
Beki Vertonghen alirekebisha kosa lake lililoipa Japan goli la kwanza kwa kupiga kichwa cha maajabu kilichowakanganya wote dakika ya (69).
Dakika tano baadaye, nguvu mpya Fellaini alifuta uongozi wa Japan na kudumusiha Ubelgiji Urusi.
Kunako dakika ya 94, Kona ya Japan iligeuka kasoro kwao kwani punde tu ilipopigwa, iligeuka kuwa hasara kwao licha ya kukusanyika kwa lango la Japan.
Thomas Meunier wa Ubelgiji alichomoka na mpira na kuanza safari iliyoishia pasi kwa Lukaku aliyempisha mwenzake Nacer Chadli kufunga kazi dhidi ya Japan!
Kwa sasa ni mechi kati ya Neymar na Eden Hazard ugani Kazan siku ya Ijumaa wiki hii.