Matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza yanaonyesha wananchi hawaridhishwi na mwenendo wa siasa na utendaji wa wanasiasa.
Idadi ya wananchi wanaokubali utendaji wa Rais John Magufuli imepungua, wakati umaarufu wa wabunge unazidi kupungua, idadi ya watu wasioshabikia vyama vya siasa inazidi kuongezeka huku uhuru wa kujieleza ukizidi kupungua, kwa mujibu wa ripoti ya matokeo ya utafiti huo iliyotolewa jana.
Hata hivyo, unaonyesha kuwa kama uchaguzi ungefanywa wakati wa utafiti huo, asilimia 55 ya wananchi wangempigia kura Rais Magufuli, idadi ambayo ni pungufu ya asilimia tatu ya ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Utafiti huo ambao ni mwendelezo wa mradi wa Sauti ya Wananchi, ulihusisha watu 1,241 waliohojiwa kati ya Aprili 15 na 24.
“Kukubalika huku kumepungua kutoka asilimia 96 mwaka 2016 na 71 mwaka 2017,” alisema mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze wakati akitangaza matokeo ya utafiti huo jana.
Alisema asilimia 55 ya wananchi wanaukubali utendaji wa Rais tangu alipoingia madarakani.
Eyakuze alisema kiwango cha kukubalika kwa kiongozi huyo mwaka 2016 kilikuwa cha juu kuliko wakati mwingine wowote katika rekodi na kwamba kimeshuka hadi rekodi ya chini tangu waanze kufanya utafiti huo mwaka 2001.
Ingawa utafiti huo haujasema sababu za kupanda na kushuka kwa umaarufu wa Rais, mwaka 2016 ni kipindi ambacho alikuwa anaunda Serikali yake akirejesha utamaduni wa kuheshimu kazi, kushughulikia ufisadi, rushwa, uzembe na uovu mwingine Serikalini.
Katika miezi ya karibuni amejikita zaidi kwenye kueleza umuhimu wa miradi mikubwa anayoitekeleza kama ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge, ununuzi wa ndege na kuhuisha mashirika ya umma.
“Kuna mambo yanafanyika mwaka huu na mwakani yatapandisha kiwango cha kukubalika kwa Rais Magufuli,” alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliyekuwa mmoja wa wazungumza wakati wa hafla ya kusoma ripoti hiyo.
“Nitazungumzia mambo makubwa matatu ambayo mwishoni mwa mwaka huu na mwaka kesho, rating ya CCM na rating ya Rais itakwenda juu.
“Wananchi wana vitu vitatu vikubwa ambavyo kwao ni muhimu; moja ni maji, mbili ni umeme vijijini (Rea-Wakala wa Nishati Vijijini), tatu, afya. Na kwenye afya wanazungumzia uwepo watumishi, zahanati na dawa upatikanaji wake ni asilimia 90.”
Alitaja pia kuboreshwa kwa huduma ya elimu na miudombinu zikiwemo barabara na reli na kuwepo kwa mkakati wa kukuza kilimo kwa ajili ya malighafi za viwandani.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na mwandishi nguli wa habari, Jenerali Ulimwengu aliyesema maendeleo ya vitu hayaondoi kiu ya wananchi kudai mabadiliko.
“Tunazungumzia ushiriki wa wananchi na wananchi ndiyo CCM,” alisema Ulimwengu.
“Majibu yake (Polepole) ni kuweka mkate mezani. Bwana Yesu au Issa bin Mariam alisema binadamu hataishi kwa mkate peke yake. Unaweza kuweka mkate na siagi, lakini kama hukumpa matumaini ya kiroho, atakuja kugeuka siku moja.
“Sawa, maendeleo ni barabara, SGR (reli ya kisasa) na mengine, lakini (kuna) spiritural development (maendeleo ya kiroho). Ukisikia mtu anasema utapigwa kama mbwa koko, huyo hana hiyo spiritual development.”
Lakini mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikuwa na maoni tofauti, akisema kushuka kwa umaarufu wa Rais kumetokana na ugumu wa maisha unaowaandama wananchi.
“Hali ya maisha kiuchumi na kimaisha inaendelea kuwa ngumu (lakini) Serikali inatoa takwimu kuwa uchumi unakua,” alisema.
“Mipango ya maendeleo ya Serikali inapitishwa na bajeti za Bunge. Kiongozi wa chama kinachoongoza Serikali anatupa taarifa maeneo ambayo kwao ni kipaumbele. Sisi wabunge tunamwambia miradi ya kipaumbele ya Serikali ya CCM si kilimo wala maji. Kwa sababu kwa fedha zilizopelekwa kwa mwaka uliopita ni asilimia 31 tu.”
Ulimwengu alikuwa mmoja wa wachangiaji wengi waliomuweka Polepole katika wakati mgumu kuhusu takwimu za kushuka kwa umaarufu wa Rais.
Wengine waliomuweka Polepole katika wakati huo ni Fatma Karume ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Vicent Mashinji (katibu mkuu wa Chadema) na Maxence Melo ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Jamii Media inayoendesha tovuti ya JamiiForums.
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Vicencia Shule alisema kushuka kwa umaarufu wa Rais kumetokana na kutotekelezwa kwa ahadi zake.
“Nguvu ya Rais imezidi kushuka. Hii ni dalili njema kwa sababu wanaona kipi kinatekelezeka na kipi hakitekelezeki,” alisema Dk Shule.
Vyama vyashuka umaarufu
Katika kipengele cha vyama kuwa karibu na wananchi, utafiti huo unaonyesha kuwa idadi ya wananchi ambao hawako karibu na chama chochote cha siasa inaongezeka.
Eyakuze alisema idadi ya wananchi wanaosema wapo karibu na CCM au Chadema imeshuka tangu mwaka 2015, CCM ikishuka kwa asilimia nne kutoka 62 hadi 58 na Chadema ikishuka kwa asilimia 11 kutoka 27 hadi 16.
Lakini pamoja na CCM kushuka, bado utafiti huo umeonyesha wananchi kwa kiasi kikubwa wanaendelea kuwaunga mkono wagombea wa CCM.
Taarifa hizo zilikuwa njema kwa Polepole ambaye alitumia nafasi hiyo kutetea amri ya kuzuia mikutano ya hadhara isipokuwa ya wabunge majimboni.
“Kuna upotoshwaji mkubwa. Mikutano ya hadhara haijapigwa marufuku ila imewekewa utaratibu zaidi ya namna ya kufanya siasa,” alisema.
“Mikutano ya hadhara tumesema, ndugu Mbowe anatoka Hai, ni mbunge ana kofia nyingi, chama chake kina uongozi. Lakini yeye kama mbunge ana jukumu la kufanya mikutano ya hadhara pale. Mtu mwingine asiingie pale Hai kufanya kazi ya siasa.”
Huku akiwalaumu wabunge wa upinzani, Polepole alisema wanachama hawaongezwi kwa kufanya mikutano ya hadhara, bali kwa mahusiano kati ya viongozi hao na wananchi.
Alisema hata CCM haifanyi mikutano ya hadhara. “Nimwekenda majimbo matatu ya upinzani ambayo mikutano ya hadhara haifanyiki. Mbowe tangu amechaguliwa amefanya mkutano mmoja Julai na Agosti 2017 lakini yeye na chama chake wanasema wamezuiwa kufanya mikutano,” alisema.
Hata hivyo, Mbowe hakutaka kujibu hoja za Polepole, akisema kufanya mikutano ya hadhara si kigezo pekee cha utendaji wa wabunge badala yake akajielekeza kwenye hoja ya kubanwa kwa Bunge na demokrasia nchini.
“Mbunge kufanya mikutano ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa wapigakura, lakini wabunge wana njia mbalimbali za kufanya kazi,” alisema Mbowe.
Uhuru wa kutoa maoni washuka
Katika suala la kupungua kwa uhuru wa kutoa maoni, Fatma alisema CCM inapaswa kujua Watanzania wengi wanataka uhuru huo.
“Ukitazama takwimu, zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanaona huo ni uhuru muhimu na wamejikita demokrasia kwenye uhuru,” alisema mwanasheria huyo wa kujitegemea.
“Sasa CCM wanasema demokrasia ni haki ya kupiga kura kwa miaka mitano. Tafsiri ya demokrasia si haki ya kupiga kura tu, ni pana. Si sawa kudharau maoni ya watu wengi.
“Unajua Serikali inadhani ikiwaambia wananchi itawapiga kama mbwa koko, itawatisha wananchi. Asilimia 18 tu hawakutaka kupigwa, lakini asilimia zaidi ya 50 wanaona kutaleta vurugu. Lakini polisi wasidhani kauli chafu au za kutisha zitawatisha wananchi kuandamana.”
Kuhusu wabunge, wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani wanavyotekeleza majukumu yao, ripoti hiyo inaonyesha wananchi wanazidi kutokubali utendaji wao.
Utafiti huo umeonyesha kuwa kuanzia mwaka 2016 wananchi wanaokubali utendaji wa wabunge imeshuka kutoka asilimia 68 hadi 44, wakati madiwani imetoka asilimia 74 hadi 45 na kutoka asilimia 78 hadi 56 kwa wenyeviti wa serikali za mitaa au vijiji katika kipindi hicho.
Wananchi pia wanaona uhuru wao binafsi wa kujieleza umepungua ndani ya miaka mitatu iliyopita baada ya utafiti kuonyesha kuwa watu sita kati ya kumi wanasema uhuru wa vyama vya upinzani umepungua.
Pia umeonyesha uhuru wa vyombo vya habari umepungua kwa asilimia 62.
Na Boniface Meena na Elias Msuya mwananchi