DC NDAGALA AWATAHADHARISHA VIJANA KUTUMIKA VIBAYA UCHAGUZI JIMBO LA BUYUNGU


Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala amewataka vijana wilayani Kakonko wasitumiwe na watu wenye nia mbaya katika kipindi hiki cha kampeni na wakati wa uchaguzi kuvuruga amani katika Jimbo la Buyungu.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na vijana waendesha bodaboda katika kata ya Kasanda wilayani humo ambapo amewataka vijana hao kufanya shughuli za maendeleo zitakazowaondoa katika umaskini na kuachana na watu wachache wenye lengo la kuvunja amani katika wilaya hiyo kwa kuchochea vurugu.

Kanali Ndagala amesema vijana wengi wamekuwa wakitumika sana katika kipindi cha uchaguzi kufanya maandamano na vurugu mbalimbali wakitumiwa na baadhi ya wanasiasa wasio waaminifu, ambapo aliwaasa vijana hao kuwa wazalendo na kusikiliza wagombea wote ili waweze kuchagua mgombea atakaye wasaidia kuleta maendeleo.

Mkuu huyo amesema serikali haitamvumilia yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa amani katika wilaya hiyo na atakayebainika anatumika vibaya hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Amesema lengo la serikali ni kuona uchaguzi huo unaisha salama na kampeni zinazofanyika ni za kistaarabu kwa kuwa amani na utulivu ndiyo nguzo bora ya kuwafanya wananchi wafanye shughuli zao.

"Mpaka sasa hatujapata taarifa ya kuwepo na vurugu katika maeneo ambayo kampeni zinaendelea niwaombe vijana msikubali kutumika kuleta vurugu wakati huu fanyeni kazi ili muweze kujikwamua kiuchumi nguvu mnazo lazima mzitumie katika kuleta maendeleo", alisema Kanali Ndagala.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo amewataka vijana hao katika msimu mpya wa kilimo kila kijana kuwa na shamba ekari moja ya pamba ili kuweza kuinua uchumi wao kwa kuwa zao hilo ni moja kati ya mazao ya biashara katika wilaya.

Hata hivyo baadhi ya vijana hao waliahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo na kuomba serikali kuendelea kudumisha amani na usalama katika wilaya hiyo.

Mmoja kati ya vijana wajasiriamali Thadeo Bitungwa amesema kwa sasa amani imeimalika tofauti na kipindi cha nyuma ambapo vijana wengi walikuwa wanatekwa na kunyang'anywa bodaboda zao, kwa sasa vitendo hivyo havipo.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post