Jumla ya wahamiaji wasio rasmi 1054 wamekamatwa katika wilaya ya Buhigwe na Kasulu mkoani Kigoma kwa kipindi cha mwaka mmoja katika oparesheni zilizofanywa na kamati ya ulinzi na usalama za wilaya hizo.
Akimkaribisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika wilaya ya Buhigwe, Mkuu wa wilaya ya Kasulu na Buhigwe Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema wameendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika wilaya hizo kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na kuendelea kupambana na vitendo vya uhalifu na uingizwaji wa silaha kiholela
Alisema kutokana na muingiliano uliopo baina ya wilaya hizo na nchi jirani ya Burundi kumekuwa na wahamiaji haramu wengi wanaoingia nchini bila vibali na wengine wamekuwa wakishirikiana na Watanzania kufanya vitendo vya utekaji kwa kutumia silaha ambapo wamejitahidi kuzuia vitendo hivyo kwa kuwakamata wote wanaoingia bila vibali nchini.
"Kwa sasa hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarika na wananchi wameendelea kuiunga mkono serikali kwa kutoa taarifa pale wanamuhofia mtu anapoingia katika maeneo yao, na tumefanikiwa katika hili na kwa sasa hakuna malalamiko yoyote ya uvunjifu wa amani kutoka kwa Wananchi", alisema Brigedia Jenerali Gaguti.
Nae Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa alilitaka jeshi la polisi kwa kushirikiana na maafisa uhamiaji kudhibiti njia ambazo sio rasmi katika wilaya ya Buhigwe kwa ajili ya kuzuia silaha zinazoingizwa nchini kiholela na watu wanaingia bila vibali.
Alisema serikali ina mpango wa kuifanya Mji wa Manyovu kuwa mji wa biashara hovyo jeshi la polisi wanatakiwa kuwa macho kwadhibiti vizuizi hivyo ili kuhakikisha wote wanaoingia nchini wanakuwa na vibali na kudhibiti silaha zilizopo katika nchi jirani kuingia nchini.
"Tunajua wilaya hii ina changamoto ya muingiliano mkubwa na ndugu zetu wa nchi jirani, leo hii Tanzania tunarekodi mbaya ya kumiliki silaha kinyume na taratibu zote hizi zinatoka nchi za jirani na kufanya uhalifu wa kutumia silaha", alieleza Waziri Mkuu.
"Lazima jeshi la polisi muandae mipaka iliyo rasmi ili kudhibiti haya uwezo huo mnao hatutaki kuona uhalifu unaendelea kuingia nchini jeshi la polisi kazi yenu ni kulinda amani na jukumu hili ni la kwenu", alisema.
Alisema serikali ya Tanzania ina mahusiano mazuri na nchi jirani hivyo mahusiano hayo yaendelee lazima utaratibu uwekwe na usalama uimarishwe.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Social Plugin