Timu ya wazamiaji leo imefanikiwa kumwokoa mtoto wa tano kati ya 12 walionasa kwenye pango nchini Thailand hatua ambayo inazidisha matumaini ya uwezekano wa kuokolewa watoto wote.
Mtoto huyo amesafirishwa kwenda kuungana na wenzake wanne walioko katika hospitali moja wakichunguzwa afya zao.
Kumekuwa na shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi walioshuhudia helikopta ikiruka kutoka eneo la tukio kuelekea hospitali.
Jana, watoto wanne waliokolewa katika operesheni iliyotajwa ya hatari na changamoto nyingi. Watoto hao na kocha wao wamekuwa katika pango hilo kwa muda wa wiki mbili sasa.
Wazamiaji wamekuwa wakiendelea na kazi hiyo kujaribu kuwaokoa watoto hao waliosalia huku wazazi wa watoto hao wakiwa katika hali ngumu kusubiri kama watawapokea wapendwa wao hao.
Mamilioni ya lita za maji yamekwisha kutolewa kutoka ndani ya pango hilo ili kurahisisha kazi ya uokoaji.
Kazi hiyo inaharakishwa kufuatia utabiri wa hali ya hewa unaodai kwamba huenda mvua kubwa itanyesha jambo ambalo litasababisha ugumu wa kazi ya kuwaokoa watoto hao.
Kiongozi wa kikosi cha uokoaji ambaye gavana wa jimbo la Chang Raiu Narongsak Osottanakorn, amesema uokoaji huo wenye mazingira ya hatari utawachukua muda zaidi.
Social Plugin