WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya usafi Coco Beach hairidhishi na amewataka viongozi wa Manispaa ya Kinondoni wajipange ili eneo hilo liweze kuvutia.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 25, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kushiriki zoezi la usafi wa eneo hilo pamoja na wananchi na watendaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ambayo hufanyika Julai 25, kila mwaka.
Waziri Mkuu ambaye aliambatana na mke wake, Mary Majaliwa, alishiriki zoezi hilo kwa kufyeka nyasi, kuzoa takataka na kupanda miti kwenye ufukwe huo. Zoezi hilo limefanyika kuanzia kwenye eneo la wafanyabiashara wa mihogo kuelekea Police Officers’ Mess.
“Eneo hili nimelitembelea, bado haliridhishi kwa usafi. Nimeenda kwenye fukwe pale na kukuta takataka nyingi zimelundikwa mahali pamoja. Ni vema Manispaa ya Kinondoni na Mamlaka zote zinazosimamia usafi ziwaratibu wanaotoa huduma na wanaopata huduma ili kuendeleza usafi wa maeneo haya nchini kote,” amesema.
Amesema Manispaa ya Kinondoni haina budi kuratibu eneo hilo kwa kupanga eneo la maegesho, la watu kupumzikia, la huduma za chakula na kuongeza kupanda miti ili wananchi waone ni maeneo mazuri yanayovutia.
“Muandae shughuli za burudani zitakazofanyika kila Jumamosi na Jumapili. Karibisheni watu wa kuleta michezo ya baharini kama vile viboti na vibaiskeli vya majini, wekeni bembea ili fukwe ivutie zaidi. Wazazi wataleta watoto wao kwenye michezo wakati wao wakikaa pembeni na kupumzika,” amesema.
Amesema vibanda vilivyoko kwenye ufukwe huo havipendezi na ikibidi waangalie uwezekano wa kuweka makontena ili kuongeza mvuto. “Vibanda hivi havileti picha nzuri sana, hivyo mnaweza kuweka makontena kutoka Pepsi au Coca-Cola ili kuleta muonekano sawia.”
“Jambo hilo linaweza kuwa ni chanzo cha mapato kwa Manispaa hii. Uongozi wa Manispaa tengenezeni haya wakati mkisubiri andiko lenu lipitishwe na muweze kupata fedha za kuboresha ufukwe huu,” amesema.
Alisema eneo jingine linalopaswa kuangaliwa katika ufukwe huo ni kuimarishwa kwa ulinzi ili watu wanaokwenda kupata huduma wasihofie usalama wao.
Waziri Mkuu amesema usafi siyo uishie kufanyika tarehe 25 tu, na akawataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye fukwe zote. “Hii ni changamoto kwenye Mamlaka ya Halmashauri ya Kinondoni, lakini pia Ilala, Temeke, Bagamoyo hadi Tanga, zinapaswa aihakikishe hizi fukwe ziwe safi,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Ally Hapi alisema mbali ya wananchi wa kawaida, walikuwepo pia askari polisi 100 na wanajeshi 150 ambao walishiriki zoezi hilo la usafi.
Alisema Manispaa ya Kinondoni wameanza kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu juu ya uboreshaji wa fukwe ya Coco kwa kuandika andiko maalum na kulipeleka Ofisi ya Rais – TAMISEMI. “Manispaa kupitia miradi ya kimkakati, tumeandaa andiko la kuomba sh. bilioni 11 za kutengeneza na kuboresha ufukwe wa Coco, na tumeshalipeleka TAMISEMI na mazungumzo yanaendelea,” alisema.
Juni 29 mwaka huu, wakati akitoa maelekezo kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha polisi kinachohamishika, Waziri Mkuu alisema: “Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anawataka Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.
Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu alitangaza kwamba Rais Magufuli ameagiza kwamba sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
Aliitaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari kwenye makutano ya barabara ya Kisasa na barabara kuu ya Dodoma Dar es Salaam na kuweka taa za barabarani kwenye barabara mpya ya mchepuko kutoka Emmaus hadi African Dream iliyojengwa ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,