'ADMIN' WA WHATSAPP ATUPWA JELA

Mwanafunzi mmoja ametumikia kifungo cha miezi mitano gerezani nchini India kufuatia ujumbe wa Whatsapp ambao anasema hakuutuma.

Taarifa zinasema mwanamume mwenye miaka 21 alishtakiwa kwa uasi kutokana na ujumbe wa 'kutusi', licha ya kwamba haijulikani wazi ujumbe huo unasema nini.

Polisi imemtuhumu mwanamume huyo kuwa msimamizi wa kundi la Whatsapp, wakati malalamiko yalipowasilishwa.

Familia yake inalalamika kwamba aliishia kuwa msimamizi wa kundi hilo baada ya wasimamizi waliokuwepo kulitoroka kundi hilo.

Junaid Khan, mwanafunzi katika mji wa Talen katika jimbo la Madhya Pradesh katikati India alikamatwa mnamo Februari 14. 

Kwa mujibu wa taarifa katika eneo hilo, mashtaka yanatokana ana ujumbe uliowasilishwa katika kundi hilo la WhatsApp ambalo yeye ni mshirika, na kuchangia yeye kushtakiwa kwa uasi.

BBC imethibitisha kuwa Khan ametumikia kifungo cha miezi mitano gerezani , licha ya kwamba ujumbe huo haujajulikana wazi.Kuna soko kubwa la WhatsApp nchini India huku kukiwa na watumiaji milioni 200 kwa mwezi nchini

Kwa mujibu wa gazeti la The Times of India, Polisi walimkamata Khan kwa kuwa msimamizi wa kundi la WhatsApp wakati kesi hiyo ilipowasilishwa kwao.

Inadhaniwa kwamba mojawapo wa wasimamizi waliokuwepo na kutoroka ndiye aliyetuma ujumbe huo, na inaarifiwa kwamba yeye pia amekamatwa.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Rajgarh amelimbia gazeti hilo kwamba wanajaribu 'kuthibitisha iwapo watu wengine pia ni wasimamizi wa kundi hilo pia'.
Umma kuchukua hatua mikononi

Kwa mujibu wa sheria ya mitandao nchini India, wasimamizi wa makundi ya mitandao ya kijamii au admins, wanaweza kufungwa gerezani kwa kusambaza ujumbe unaoonekana kuwa ni tusi kidini au kisiasa.

Huku kukiwa na watumiaji milioni 200 kwa mwezi nchini, mara nyingi watu wengi hukamatwa kutokana na uhalifu katika WhatsApp. Maafisa wanasema hatua zimeidhinishwa kuzuia watumaiji mitandao ya kijamii kuchochea ghasia.

Wiki iliyopita, kampuni hiyo inayomilikiwa na Facebook imetangaza itapunguza kiwango ambacho ujumbe unaweza kusambazwa India, ili kuzuia kusambaa kwa taarifa za uongo katika jukwaa hilo.

Hatua hiyo imetolewa baada ya visa kadhaa vya raia kuchukua hatua mikononi kuhusishwa na ujumbe uliosambazwa katika makundi ya WhatsApp.
Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post