Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BASHE ABAINI WAZAZI WANAENDELEA KUTELEKEZA WATOTO KIGOMA...AMPA WATATU MBUNGE


Mbunge wa jimbo la Nzega mjini Hussein Bashe na Mbunge wa Viti maalumu wa vijana mkoa wa Kigoma Zainabu Katimba, akikabidhi fedha za kuwanunulia nguo za shule za watoto waliotelekezwa na wazazi wao kwa mwalimu mkuu msaidizi shule ya msingi Churazo mkoani Kigoma Silvia Mgina. Picha na Rhoda Ezekiel Kigoma. 
***
Tatizo la wazazi kutelekeza watoto wilayani Kakonko mkoani Kigoma limekuwa sugu jambo ambalo linasababisha watoto wengi kukosa haki yao ya kupata elimu kama watoto wengine.

Hayo yalibainika jana wakati wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Buyungu, baada ya Mbunge wa jimbo la  Nzega mjini Hussein Bashe kubaini kuwepo kwa watoto watatu katika Kijiji cha Churazo wilayani humo,January Magaruka (13), Erick Magaruka (11),John Magaruka (9) waliotelekezwa na wazazi wao na kulelewa na askari mgambo katika kijiji hicho. 

Bashe aliwachukua watoto hao na kuwakabidhi kwa Mbunge wa Vijana wa Mkoa wa Kigoma , Zainabu Katimba na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo kuomba wawalee watoto hao na kuhakikisha wanapata elimu na malezi bora.

"Nikienda katika mikutano ya kampeni huwa napenda kuzungumza na watoto ili kujua matatizo waliyonayo,nimebaini watoto kadhaa Wilayani Kakonko wamekimbiwa na wazazi wao na wengine wanaishi katika mazingira magumu, jamii na viongozi wa Wilaya hii wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha watoto wa aina hii wanapatiwa elimu", alisema Bashe.

Naye mbunge wa viti maalumu vijana wa Mkoa wa Kigoma Zainabu Katimba aliahidi kuwalea watoto hao kama watoto wake kwa kuwasiliana na Mwalimu huyo ili watoto hao waendelee na elimu kama watoto wengine.

Zainabu alisema wazazi wanatakiwa kubadilika na kwamba ugomvi wao wasiwahusishe watoto na wajitahidi kuhakikisha watoto wanapata elimu kwa kuwa elimu ni urithi mkubwa kwa watoto katika kujikwamua na umaskini.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Churazo ,Silvia Mgina, aliahidi kuwachukua Watoto hao na kuwaandikisha darasa la kwanza 2019 na mtoto mwenye umri mkubwa watamuweka katika mpango wa elimu ya watu wazima katika shule hiyo.

 Alisema tangu mwaka 2014 hadi sasa wamepokea watoto 128 waliotelekezwa na wazazi wao na kushindwa kupelekwa shule lakini sasa wamewaandikisha watoto hao.

Hata hivyo Baba mdogo wa watoto hao Kazena Magaruka alisema wazazi wa watoto hao Maneno Magaruka na Christina Magaruka waliwakimbia watoto wao kutokana na mwanaume huyo kumuacha mke wake na kwenda kutafuta maisha mkoani Kagera na kuoa mwanamke mwingine na kumuacha mama huyo na watoto peke yake.

Alisema wawili hao walikuwa na ugomvi baada ya mwanaume huyo kwenda kuoa mke mwingine na mwanamke huyo aliamua kuwakimbia watoto hao na kwenda kuolewa na mwanamume mwingine na kupelekea watoto hao kuendelea kuishi katika mazingira magumu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alisema changamoto ya wazazi kukimbia familia zao limekuwa ni tatizo, na kueleza kuwa serikali imeandaa utaratibu wa kuwakamata wale wote wanaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule na kuwachukulia hatua.

Alisema serikali inatoa elimu bila malipo, kazi ya wazazi ni kuwanunulia sare za shule na kuhakikisha wanahudhuria shule na kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapelekwa shule.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com