MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo Agosti 3 (Ijumaa) mwaka huu ,anatarajia kuwaapisha viongozi wateule Jokate Mwegelo na Zainab Kawawa.
Akizungumzia juu ya hafla hiyo fupi ,Ndikilo alisema inatarajiwa kufanyika asubuhi katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa huyo .
Alisema viongozi hao bado ni vijana ambao anaamini kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi ya awamu ya tano wilaya ya Kisarawe na Bagamoyo zitapiga hatua zaidi .
Alisema kikubwa ni kwenda pamoja na kuinua sekta ya viwanda na kuhimiza kilimo cha biashara cha korosho kwenye maeneo yao .
“Katika miaka ya 1995 zao la korosho lilikuwa juu wilaya ya Kisarawe ,hivyo endapo tutaendelea kulipa msukumo kwa kulifufua, itasaidia kuinua zao hilo tegemezi la kibiashara katika mkoa wa Pwani”alisema Ndikilo.
Hata hivyo Ndikilo alisema, mkoa huo unatekeleza vyema ujenzi wa viwanda na wawekezaji hivyo kutokana na uteuzi wa Rais Dk. John Magufuli anashukuru kuongezewa nguvu ya viongozi wengine ambao ni vijana katika wilaya hizo.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza ,kwa upande wa Kisarawe pia lipo tatizo la maji ambapo juhudi kubwa zitatakiwa katika kusimamia mradi wa bilioni kumi ambao utatoa maji Mloganzila hadi Kisarawe.
” Jokate ni kijana mwenye kipaji ,alishapitia chipukizi ,umoja wa vijana na masuala mengine ya kimaendeleo ,naamini ataweza kukimbiza gurudumu la maendeleo kwa kusimamia kutatua changamoto zilizopo Kisarawe ikiwemo mkandarasi huyo wa mradi wa maji Mloganzila-Kisarawe”
Pamoja na hayo ,Ndikilo aliwataka wakuu wa wilaya mkoani hapo ,kuwatumikia wananchi ,kusimamia miradi ya maendeleo na mapato katika maeneo yao .
Alieleza kwa umoja wa wakuu wa wilaya ,watendaji ,chama cha Mapinduzi na kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao hakuna litakaloshindikana.
Wateule hao ni miongoni mwa waliteuliwa walioteuliwa na Rais Dk.John Magufuli Julai 28 mwaka huu.
Na Mwamvua Mwinyi,pwani
Social Plugin