WATANZANIA wametakiwa kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika kufanya shughuli za usafi wakati maadhimisho ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kutimiza miaka 54 tangu kuanzishwa kwake.
JWTZ linatarajia kufikisha miaka 54 ifikapo Septemba 1 mwaka huu.Jeshi hilo lilianzishwa mwaka 1964.
Akizungumzia sherehe hizo Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ Kanali Ramadhani Dogoli amesema katika maadhimisho hayo ya mwaka huu jeshi limeanza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na kujishughulisha katika michezo.
“Itakumbukwa kila mwaka inapofika tarehe hiyo bada ya kubadilishwa jina kutoka Tanganyika Rifle (TR) kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
"Na sherehe hizo kila mwaka tumekuwa tukifanya shughuli za kijamii kwa kufanya usafi kwenye maeneo ya kambi zote za jeshi na kushiriki katika michezo,”amesema.
Amefafanua michezo inayoendelea kuchezwa ni mpira wa miguu,Pete,wavu, golf na mingine na kwamba timu za jeshi na za uraiani ndizo zinashiriki michezo hiyo.
Kanali Dogoli amefafanua shughuli hizo zilianza kufanyika Agosti 27 mwaka huu na kwamba zitaendelea hadi siku kilele cha sherehe hizo.
Hivyo limesisitiza umuhimu wa watanzania wote wenye mapenzi mema kungana kuadhimisha siku hiyo kwa kujitokeza kufanya usafi katika maeneo yao wanayoishi na kuyaweka katika hali ya usafi.