Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATUMBI AZUIWA KUINGIA DRC KUKABIDHI FOMU ZA KUGOMBEA URAIS

Kiongozi wa upinzani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Moise Katumbi, amezuiwa kurudi nchini humo kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo Desemba mwaka huu.


Serikali ya Congo imemzuia Gavana huyo wa zamani wa Jimbo la Katanga anayeishi uhamishoni nchini Afrika Kusini kurudi nyumbani kuwasilisha fomu za kugombea urais.


Katumbi aliondoka DRC Mei mwaka juzi na kuelekea Afrika Kusini kwenda kupata matibabu baada ya kushutumiwa kuwaajiri wapiganaji ambapo pia alihukumiwa bila yeye kuwapo kwa kosa la kuuza viwanja kinyume cha sheria na kupewa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela.


Katumbi aliomba ruhusa kuingia nchini leo asubuhi kuwahi kuwasilisha makaratasi yake ya uteuzi wa chama kuwa mgombea urais kwa tume ya uchaguzi nchini humo.


Maofisa wa polisi mjini Lubumbashi wameweka vizuizi katika barabara kuu na usalama umeimarishwa ndani na katika maeneo yaliyo karibu na uwanja wa ndege. Pia kuna mipango ya kuzifunga njia za ndege ili kuizuia ndege ya Katumbi isitue DRC.


Waziri wa habari Lambert Mende amesema aliyekuwa Gavana huyo wa zamani kutoka jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini atakamatwa iwapo atajaribu kuingia nchini kwa ndege za abiria.


Kiongozi mwingine wa upinzani Jean-Piere Bemba amewasili DRC siku ya Jumatano baada ya kuondoka kwa zaidi ya muongo mmoja.


Bemba aliwasilisha fomu yake ya kugombea urais hapo jana Alhamisi.


“Naweza kuthibitisha nilikuwa na kadi ya kupiga kura, na nimewasilisha nyaraka zote,” Shirika la Habari la AFP limemnukuu Bemba akizungumza nje ya makao makuu ya Tume ya Uchaguzi.


Hata hivyo, chama tawala cha PPRD kimesema hafai kugombea kwa sababu alishtakiwa kwa kosa la jinai rushwa katika mahakama ya kimataifa ya jinai ICC. Ingawa amekataa rufaa kupinga kesi hiyo.


Katumbi ni kiongozi pekee wa upinzani nchini DRC ambaye ana ushawishi mkubwa na ufuasi mkubwa miongoni mwa raia wa Congo na anayetarajiwa kumpa Rais Joseph Kabila ushindani mkali endapo atawania tena. Alitangaza kutaka kuwania urais mwaka juzi, kabla ya uchaguzi huo kuahirishwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com