Mabasi 12 yanayofanya safari za kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali leo Jumatatu Agosti 6, 2018 yamesitisha safari zake mpaka yatakapotengenezwa baada ya kubainika kuwa na kasoro katika mfumo wa usukani.
Akizungumza leo wakati akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu ukaguzi wa mabasi katika msafara wa mafunzo ya usalama barabarani kuelekea mkoani Tanga, mrakibu wa Jeshi la Polisi, Abel Swai amesema mabasi hayo hayataruhusiwa kuondoka mpaka yatengenezwe.
Swai ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma kikosi cha usalama barabarani, amesema changamoto kubwa ya mabasi yaliyo mengi ni tatizo la mikono ya usukani.
Amesema wanaangalia zaidi kama basi linaweza kukata kona vizuri, liwe na mneso na kubaini changamoto wanazokutana nazo, hasa kwa mabasi yanayosafiri umbali mrefu akibainisha kuwa kama yatabainika upungufu unaweza kuwa chanzo cha ajali.
"Ukaguzi huu unafanyika kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani sura ya 168 ya mwaka 2002 fungu la 39 ambayo imebainisha mambo ambayo ni ya muhimu katika gari ambayo kama yatakuwa hayafanyi kazi halitaruhusiwa kuendeshwa," amesema.
Mkaguzi wa mabasi wa kikosi cha usalama barabarani katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT), Ibrahim Samwix amesema kwa taratibu za Sumatra, mabasi hayo yanatakiwa kufungwa vipuri vipya na baada ya ukaguzi yataruhusiwa kuendelea na safari.
“Mabasi yote yana abiria na tunawapa muda wa kuyatengeneza yasizidi masaa mawili, kama wakishindwa itabidi washushe abiria watafutiwe usafiri mwingine," amesema Samwix bila kutaja majina ya mabasi hayo.
“Changamoto kubwa hata waliopo ndani ya mabasi si mafundi maana mkiingia kukagua basi huko chini wao hawaoni tatizo lolote,” amesema.
“Wanajua kutengeneza lakini hawawezi kubaini tatizo na hawataki kujifunza. Sisi tupo tayari kuwafundisha ila huwa hawajitokezi.”
Social Plugin