Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa (CCM) Nape Nnauye ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mtama amesema Chama Cha Mapinduzi kilimpitisha Rais John Magufuli kwa maksudi kugombea urais na sio bahati mbaya kutokana na nchi ilipokuwa imefikia na hawajutii uamuzi walioufanya katika mchakato wa kumpitisha rais Magufuli.
Nnauye aliyasema hayo jana katika kijiji cha Mbizi wilayani Kakonko wakati akimnadi mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Buyungu Christopher Chiza.
Alieleza kuwa wakati wanamtafuta mgombea wa urais awamu ya tano walitaka mgombea ambaye atakwenda kudhibiti fedha za serikali asiyecheka na wezi kwa ajili ya kuziba mianya yote ya rushwa.
Kufuatia kauli hiyo Nnauye alisema kutokana na mambo yanayofanywa na rais Magufuli wapinzani wanatakiwa kuacha siasa walizokuwa wakizifanya wakati wa uongozi wa awamu ya nne na kwamba wasikariri siasa na wasipofanya hivyo wanachama na viongozi wao watawakimbia.
Alisema kazi anayoifanya Rais ni kuhakikisha anadhibiti mianya ya rushwa na wananchi wanapata maendeleo akibainisha kuwa wanao ilalamikia serikali ya awamu ya nne ni wale waliozoea kuiba fedha za wananchi ambao kwa sasa wamebanwa.
"Huyu ndiyo kiongozi anayehitajika na kwa kweli hakuna jambo ambalo Watanzania wanaweza kumsema vibaya Rais, lazima wapinzani mkubaliane na hali iliyopo, lengo la kuwepo na mfumo wa vyama vingi ni kuikosoa serikali inapofanya vibaya na sio kuipinga serikali inapofanya maendeleo, mkikariri siasa za awamu ya nne wananchi watawashangaa kwa kweli", alisema Nnauye.
Hata hivyo aliwaomba wananchi wa jimbo la Buyungu kumchagua kiongozi mwenye sifa tano ambazo, ni kiongozi anayewajua ,mtu wanayemfahamu kutokana na mazuri yake aliyoyatenda, mtu anayejua matatizo ya wananchi, mtu anayejua wapi pakutatulia matatizo ya wananchi na awe na uwezo wa kwenda kuchukua fedha na kuwaletea maendeleo.
Alisema endapo watamchagua kiongozi wa upinzani hana sifa hizo kwa kuwa hana rais ambaye atakwenda kazungumza naye lugha moja na endapo watamchagua atahama chama na kuiongezea serikali bajeti ya kuingiza kwenye uchaguzi mpya.
Alisema Chiza ni kiongozi anayefahamu matatizo ya Wanakakonko na anajua ni wapi pakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo yao na kuwaletea yale yote atakayo yaahidi kwa kuwa anaahidi mambo yaliyopo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha Mgombea Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Christopher Chiza aliendelea kuwaomba wananchi wamchague wakati akiendelea kuwaahidi kutatua tatizo la ukosefu wa maji na kuwaletea umeme kupitia REA awamu ya tatu katika vijiji vyote ambavyo havijapata umeme.
Alisema uwezo wa kwenda kuwasemea wananchi wa Kakonko anao na kuomba Wananchi hao wamchague ilikusudi aweze kwenda kukamilisha yale yote ambayo hayakufanyika kwa miaka mitatu iliyopotea na hii iliyo baki.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Nape Nnauye akiwahutubia wananchi wa jimbo la Buyungu wakati akimnadi Christopher Chiza -Picha na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Social Plugin