Hofu imetanda miongoni mwa wakazi wa vijiji vya Misasi, Isakamawe na Mabuki wilayani Misungwi mkoani Mwanza baada ya maiti za wanawake wanne kuonekana huku zikiwa hazina baadhi ya viungo.
Miili hiyo imeokotwa maeneo tofauti ikiwa na alama zinazoonyesha walinyongwa kabla ya kufariki.
John Makoye mkazi wa Isakamawe aliyeshuhudia maiti ya marehemu hao ametaja baadhi ya viungo vilivyonyofolewa kuwa ni ulimi, matiti na sehemu ya siri.
Akizungumza leo Ijumaa Agosti 3, 2018 kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amewataja waliouawa kuwa ni Angelina Lumala (45) mkazi wa kijiji cha Isakamawe, Kundi Laurent (35) na Mariamu Manila (30) wote wakazi wa kijiji cha Misasi na mmoja aliyetambulika kwa jina la Ngole (43) mkazi wa Kitongoji cha Bujingwa kijiji cha Mabuki.
Amesema polisi tayari inawashikilia kwa mahojiano watu watatu ambao hakuwa tayari kuwataja majina waliokutwa kwenye mapori ambako miili hiyo ilikutwa.
Akizungumza na familia za marehemu baada ya kuzitembelea, Kamanda Msangi amewaomba wananchi wenye taarifa zitakazosaidia kuwanasa wauaji kujitokeza kusaidiana na polisi.
"Si tukio la kawaida watu wanne kutoka maeneo na vijiji tofauti kuuawa katika mazingira yanayofanana. Kuna dalili za mauaji haya kuhusishwa na imani za kishirikina zinazotokana na ramli chonganishi. Tutawasaka na kuwatia mbaroni wote waliohusika na matukio haya,” amesema Kamanda Msangi.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Misungwi, Marco Peter amewataka akina mama wanaokwenda porini kukata kuni kuchukua tahadhari na kuwa katika makundi na ikiwezekana waongozane na waume zao.
“Viongozi wa vitongoji na vijiji nao wanapaswa kuimarisha vikundi vya ulinzi wa jadi maarufu kama Sungusungu katika maeneo yao kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao,” amesema.
Na Twalad Salum, Mwananchi
Social Plugin