Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MDOLWA AWAHAKIKISHIA WANANCHI CCM KUKAMILISHA AHADI ZAKE 2020


Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi CCM taifa Edmundi Mdolwa amewahakikishia  wananchi kuwa serikali ya awamu ya tano  itahakikisha ifikapo mwaka 2020 itakuwa imekamilisha ahadi zote zilizoahidiwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Amebainisha kuwa CCM katika uchaguzi mkuu huwa inaingia mkataba na wananchi kuomba ridhaa ya kupewa kuiendesha serikali katika kuleta maendeleo na katika chaguzi ndogo chama hicho kinahakikisha kinapata mgombea atakayeungana na viongozi waliopewa ridhaa ya kuendesha serikali huku akiwaomba wananchi kuchagua mgombea wa chama hicho awaletee maendeleo.


Ameyasema hayo leo katika kijiji cha Kabale kata ya Gwarama Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma, wakati akimnadi mgombea wa chama hicho.


Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa awamu ya tano serikali kupitia Chama tawala cha CCM kimeweza kutekeleza mambo ambayo waliingia mkataba na wananchi kupitia Ilani ya Chama hicho, ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kujenga barabara, vituo vya afya na kukamilisha miradi ya maji.

Ameeleza mpaka sasa serikali imeweza kuinua uchumi wa Tanzania kwa kununua ndege kubwa za kisasa zitakazokwenda nje ya nchi, kufanya marekebisho kwa kujenga miundombinu mbalimbali lengo ikiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.


"Nimekuja kumnadi mgombea huyu nimeagizwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na ndio anayepitisha fedha za miradi, niwaombe wananchi mumchague mgombea huyu kwa kuwa ana uwezo wa kwenda kumuomba kiongozi ambaye itikadi yake na yeye ni moja ", alisema Mdolwa.


Alieleza kuwa CCM ni chama kinachoaminiwa na wananchi kutokana na kazi kubwa anayoifanya Rais ndiyo maana viongozi wa vyama vya upinzani wanahama vyama vyao na kuunga mkono serikali ya awamu ya tano.


Naye aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini Dkt Siriri Chami aliwaomba wananchi wa Kakonko wasifanye makosa waliyoiyafanya 2015 ambayo yanaweza kuwagharimu kukosa maendeleo katika wilaya hiyo na kuwa majuto kwao.

Awali akiomba ridhaa kwa wananchi waweze kumchagua mgombea mbunge kwa jimbo la Buyungu Eng.Christopher Chiza alisema shida za wananchi anazitambua ikiwemo zahanati na changamoto ya maji ambayo ameahidi kutatua changamoto hiyo endapo watamchagua atafuatilia mipango iliyoshindwa kukamilika.

Alisema ipo miradi ambayo imepitishwa na serikali ikiwemo milioni 628 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mitaani katika wilaya lakini imekosa wafuatiliaji kwa sababu palikuwa hakuna mtu wa kufuatilia na Mbunge aliyekuwepo alishindwa kufanya hivyo, na Wananchi wa Kakonko wamekosa maendeleo kutokana na usimamizi mbovu wa miradi.
Na Rhoda Ezekiel Kigoma.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com