Polisi mkoani Kagera inamshikilia mwalimu Respicius Patrick wa shule ya msingi Kibeta akituhumiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano, Siperius Eradius.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi alisema kifo cha mwanafunzi huyo kilitokea jana akipelekwa hospitali.
Alisema Patrick (50), ambaye ni mwalimu wa nidhamu anadaiwa kumpiga mwanafunzi huyo akihusishwa na upotevu wa mkoba wa mwalimu Herieth Gerard (46) uliokuwa na Sh75,000 na vitambulisho vyake.
Hata hivyo taarifa kutoka eneo la tukio na kwa baadhi wa wanafunzi wa shule hiyo, wakati mwanafunzi huyo akiendelea kuadhibiwa, pochi ikiyodaiwa kuibwa ilipelekwa shuleni hapo na mwendesha pikipiki aliyemsafirisha mwalimu Herieth wakati akienda kazini, akidai aliisahau.
Baba wa mwanafunzi huyo, Justus Balilemwa alisema alimchukua mtoto huyo kituo cha watoto yatima cha Ntoma baada ya mama yake kufariki dunia akijifungua.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa Mkoa wa Kagera, Dk John Mwombeki alisema uchunguzi wa awali wa mwili wa mwanafunzi huyo unaonyesha alama zinazohusishwa na kupigwa.