Imeelezwa kuwa zaidi ya wanafunzi 17,303 hawajakidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya elimu ya juu na Bodi ya Mikopo nchini kutokana na kutokamilisha viambata muhimu vinavyohitajika hali iliyopelekea kuongezwa siku nyingine 15.
Afisa Mawasiliano mwandamizi kutoka Bodi ya Mikopo, Veneranda Malima amesema kuwa mpaka kufikia Julai 31, 2018 ambapo ndiyo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa wanafunzi kutuma maombi kwa ajili ya kupatiwa mkopo, wanafunzi 88,502 walituma maombi na 78,290 pekee ndio waliokidhi vigezo mpaka sasa.
Kufuatia takwimu hizo zaidi ya wanafunzi 17,303 hawajakamilisha vitu muhimu vya kuambatanisha katika fomu za kuomba mikopo ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya wadhamini hivyo kupelekea bodi kuongeza muda wa siku kumi na tano.
“Kwasasa hatupokei maombi mapya, lakini muda tulioongeza ni kwa wale waombaji ambao hawakukamilisha viambatanisho muhimu kutokana na wengi kutokuweka vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya wadhamini”, amesema Malima.
Mei 10, 2018 Bodi ya mikopo ilianza rasmi kupokea maombi kutoka kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya juu na tarehe 31 Julai, 2018 Bodi ilifunga zoezi la udahili wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Kiasi cha shilingi Bilioni 427.5 kimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2018/2019 ambazo ni kwa wanafunzi wenye mikopo hivi sasa , na waombaji wapya ambao wana sifa za kujiunga na kozi za shahada katika vyuo vikuu nchini.
Social Plugin