Picha : AGPAHI YAENDESHA WARSHA KWA WAJUMBE WA KAMATI YA BUNGE - UKIMWI DODOMA...WABUNGE WAIPONGEZA

Asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) inayojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi na Ukimwi imeendesha warsha kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI kuwaeleza kuhusu shughuli wanazotekeleza pamoja na kujadiliana namna ya kushirikiana kufikisha huduma za VVU na Ukimwi kwa wananchi.


Warsha hiyo imefanyika Alhamis Septemba 13,2018 katika ukumbi wa Msekwa bungeni Dodoma na kukutanisha pamoja wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI,maafisa kutoka AGPAHI na wadau wa AGPAHI.

Awali akizungumza katika warsha hiyo,Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt, Sekela Mwakyusa alisema wameona ni vyema kukutana na wajumbe wa kamati hiyo ili kuwaeleza shughuli zinazofanywa na AGPAHI.

“Suala la VVU na Ukimwi ni suala mtambuka,tumekutana nanyi kwa ajili ya kuwaeleza kazi tunazofanya katika mikoa sita nchini ambayo ni Mwanza,Mara,Tanga,Shinyanga,Geita na Simiyu lakini pia kujadili maeneo ambayo AGPAHI na serikali tunaweza kushirikishana katika kuboresha huduma za VVU na Ukimwi”,alieleza Dk. Sekela.

“Tunachotaka sisi ni huduma ziwafikie wananchi wengi zaidi,watu wapime na kutambua hali ya afya zao na wale watakaokutwa na maambukizi ya VVU waanze mara moja kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU,tunataka wabunge waelewe na kuupeleka huu ujumbe kwa wabunge wenzao bungeni lakini pia kwa wananchi wanaowaongoza”,aliongeza Dk. Sekela.

Alisema kwa kuwa lengo la AGPAHI ni kuhakikisha hakuna mtoto anayepata Ukimwi hivyo kuwezesha watoto wote na familia zao kuishi maisha yenye matumaini,nuru na upendo na kwamba asasi inaendelea kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za matunzo na tiba za VVU kwa watoto wachanga,vijana na watu wazima.

Alibainisha kuwa mpaka sasa AGPAHI imefanikiwa kuwafikia Watanzania 240,000 ambao wanapata huduma za VVU na Ukimwi kati yao 16,000 ni watoto.

Dk. Sekela aliwaomba wabunge kuishinikiza serikali kuongeza fedha kwenye masuala ya Ukimwi ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Kwa upande wao Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati,Mheshimiwa Oscar Mukasa waliipongeza asasi ya AGPAHI kwa jitihada inazozifanya katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi huku wakiomba asasi  hiyo iongeze maeneo ya kutekeleza mradi huo.

“Serikali inatambua kazi mnazofanya katika kuwahudumia Watanzania,naomba tuendelee kushirikiana”,alisema Mukasa.

“AGPAHI wamesaidia sana kuboresha huduma kwenye vituo vya afya,wanatoa elimu na misaada mbalimbali,wamekuwa wakifuatilia sana kuhusu masuala ya VVU na Ukimwi kwenye vituo,tunachotakiwa kufanya ni kutoa elimu zaidi kwa jamii kuhusu VVU na Ukimwi”,alisema Richard Ndassa mbunge wa Sumve na Joyce Sokombi mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mara.

“Kwa kuwa mnafanya vizuri katika mikoa mliyopo na kila mtu anawasifia tunaomba pia mfike kwenye mikoa mingine kwani tunahitaji sana huduma zenu”,alisema Frances Mwalongo mbunge wa jimbo la Njombe Mjini na Makame Mashaka Foumu wa Kijine Zanzibar.

Naye Mkuu wa mkoa wa Mwanza,John Mongella alisema mafanikio ya AGPAHI ambao wamekuwa wadau wakubwa wa sekta ya afya yanatokana na ushirikiano uliopo kuanzia ngazi ya halmashauri za wilaya na mikoa.

Warsha hiyo imekwenda sanjari na maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na AGPAHI katika kutekeleza miradi ya Ukimwi.

Hii ni mara ya kwanza kwa asasi ya AGPAHI kukutana na wajumbe wa kamati ya bunge inayohusu masuala ya Ukimwi ingawa mwaka 2016 asasi hiyo ilikutana na wabunge kutoka kwenye mikoa ambayo wanatekeleza miradi mbalimbali ya Ukimwi kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) chini ya Vituo vya Kudhibiti Magonjwa na Kinga (CDC).

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Oscar Mukasa ambaye ni mbunge wa Jimbo la Biharamulo akifungua warsha kuhusu shughuli zinazotekelezwa na  Asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) iliyofanyika Septemba 13,2018  katika Ukumbi wa Msekwa bungeni Dodoma Septemba 13,2018 - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Mheshimiwa Oscar Mukasa akizungumza wakati wa warsha hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dk. Sekela Mwakyusa. Kulia ni Katibu wa kamati hiyo, Happiness Ndalu.
Mheshimiwa Oscar Mukasa akizungumza wakati wa warsha hiyo.
Mkurugenzi wa Asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), Dk. Sekela Mwakyusa akijitambulisha kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI. 
Dk. Sekela akielezea historia ya asasi ya AGPAHI iliyoanzishwa mwaka 2011 kwa msaada wa asasi ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) katika mikoa mitatu ya Shinyanga,Geita na Simiyu kisha mwaka 2016 mikoa mitatu ya Tanga,Mara na Mwanza ikaongezewa na kufanya AGPAHI kufanya shughuli zake katika mikoa sita nchini.
Dk. Sekela akiwaeleza Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI  jinsi AGPAHI inavyozingatia miongozo ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto katika mapambano ya VVU na Ukimwi kwa kuhakikisha kuwa watoto,wanawake na familia zao kwa ujumla wanapata huduma bora za VVU na UKIMWI.
Dk. Sekela  akielezea kuhusu mafanikio ya AGPAHI ambapo alisema kupitia programu za AGPAHI watoto zaidi ya 35,000 waliozaliwa na mama wenye VVU walizaliwa bila kuwa na maambukizi ya VVU kutokana na huduma bora za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI wakiandika dondoo muhimu wakati Dk. Sekela akiwasilisha mada kuhusu shughuli zinazofanywa na AGPAHI.
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI wakimsikiliza Dk. Mwakyusa.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza,John Mongella akitoa ushuhuda wa kazi nzuri zinazofanywa na AGPAHI katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza,John Mongella alisema AGPAHI wamekuwa wadau wakubwa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI mkoani Mwanza.
Wajumbe wa bodi ya AGPAHI na maafisa kutoka AGPAHI wakiwa ukumbini.
Mtoa huduma kutoka kituo cha Tiba na Matunzo katika kituo cha afya Makorola mkoani Tanga Rukia Majatta ambaye anaishi na VVU kwa miaka 28 sasa akielezea huduma zinazolewa na AGPAHI na kuwataka waliopata maambukizi ya VVU kuzingatia matumizi ya dawa za kufubaza makali ya VVU.
Kijana Edson Justin kutoka mkoani Shinyanga  ambaye ni muelimisha rika kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI akielezea huduma zinazotolewa na AGPAHI kwa watoto na vijana waliopata maambukizi ya VVU.
Mtoa huduma kutoka mkoani Simiyu,Michale Bundala ambaye anaishi na maambukizi ya VVU pamoja na mke wake akielezea kuhudu huduma zinazotolewa na AGPAHI na jinsi yeye na mkewe walivyozaa mtoto ambaye hana maambukizi ya VVU. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kahama,Underson Msumba akifafanua kuhusu huduma zinazotolewa na AGPAHI katika halmashauri yake.
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Dk. Seif Shekalaghe akiwashukuru AGPAHI kwa jitihada wanazofanya juu ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Azza Hilal Hamad ambaye ni mjumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI akizungumza wakati wa warsha hiyo na kupongeza kazi zinazofanywa na AGPAHI katika kuwahudumia watanzania.
Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI,Raphael Chegeni ambaye ni mbunge jimbo la Busega akiishukuru AGPAHI kwa kuendelea kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
Katikati ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa ambaye ni mjumbe wa wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.
Katikati ni Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Mheshimiwa Frances Mwalongo ambaye ni mbunge wa jimbo la Njombe Mjini akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.
Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI,Mheshimiwa Richard Ndassa ambaye ni mbunge wa Sumve akizungumza wakati wa warsha hiyo na kuomba serikali na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI.
Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI,Mheshimiwa Joyce Sokombi ambaye ni mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mara akizungumza wakati wa warsha hiyo na kuipongeza AGPAHI kwa huduma inazotoa.
Kulia ni mbunge wa Kijine Zanzibar, Mheshimiwa Makame Mashaka Foumu akiomba AGPAHI kuongeza mikoa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya VVU na UKIMWI.
Mjumbe wa Bodi ya AGPAHI, Ringo Fred akiomba serikali kuboresha barabara za vijijini ili kurahisisha kuyafikia maeneo mengi zaidi kwa ajili ya kutoa huduma za VVU na UKIMWI.
Warsha inaendelea.
Picha ya pamoja washiriki wa warsha hiyo.
Picha ya pamoja maafisa wa AGPAHI na wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI.
Septemba 12,2018 katika viwanja vya Bunge Dodoma : Maafisa wa AGPAHI,Wajumbe wa bodi ya AGPAHI na wadau wa AGPAHI wakiwa katika picha ya pamoja kwenye banda la maonesho ya shughuli zinazofanywa na AGPAHI.
Katikati ni Meneja wa Huduma za Kitabibu kutoka AGPAHI, Dkt. Sarah Matemu akimwelezea mheshimiwa mbunge Philipo Mulugo (kushoto) kuhusu shughuli zinazofanywa na AGPAHI kuhusu mapambano dhidi ya VVU. Kulia ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza,Cecilia Yona.
Wabunge wakiwa katika banda la maonesho la AGPAHI.
Mratibu wa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka AGPAHI, Felix Muchira akitoa ufafanuzi wa huduma zinazotolewa na AGPAHI katika vituo vya tiba na matunzo.
Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Shaurimoyo Zanzibar Mheshimiwa Mattar Ali Salum akisikiliza kwa umakini maelezo kutoka kwa Meneja wa Huduma za Kitabibu AGPAHI, Dkt. Sarah Matemu kuhusu huduma za VVU na UKIMWI zinazotolewa na AGPAHI.
 Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post