Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia amesema kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere katika Ziwa Victoria ni ajali ya kujitakia.
Mbatia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 21, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam, akisema zaidi ya asilimia 96 ya majanga yanasababishwa na wanadamu, asilimia nne tu ndiyo majanga asilia.
Mbunge huyo wa Vunjo akizungumzia kiundani kuhusu majanga, alieleza aina tatu za majanga na kubainisha kuwa kuzama kwa meli hiyo jana mchana Septemba 20, 2018, ni janga lililokuwa likijulikana, wahusika walikuwa wakijua.
Amesema Taifa linapopata janga moja kubwa, hutoa elimu ya kujikinga ili janga kama hilo lisijitokeze tena.
“Ukiacha ajali hii ya kivuko, meli za MV Spice Islanders na MV Bukoba ambazo zote zilizama, zilikuwa elimu tosha na hizi ajali za meli kuzama hazikupaswa kutokea tena,” amesema Mbatia.
“Ukikusanya ajali hizi ukiwa na takwimu sahihi za kutosha na rejea ya majanga unaweza kujua jinsi ya kuokoa raia, kulinda raia ili yasitokee tena majanga badala ya kulalamika na kunyoosheana vidole, kushikana mashati.”
Amesema ajali za aina hiyo zinapotokea, wengi huishia kutoa pole jambo ambalo halisaidii.
Amesema iwapo mapendekezo yaliyotolewa na Jaji Robert Kisanga baada ya kutokea kwa ajali ya MV Bukoba mwaka 1996, ufumbuzi wa nini kifanyike inapotokea ajali ya aina hiyo ungekwishapatikana.
Mbatia ameshauri kuanzishwa kwa sheria ya wakala wa usimamizi wa maafa kwa lengo la kuwalinda na kuwakinga wananchi.
"Kupanga ni kuchagua, kama walikuwepo wa Chadema walikufa, wa CUF walikufa wa NCCR walikufa, kitengo hicho licha ya kupigiwa kelele hakikuundwa na wanaozungumza ni Polisi, Mkuu wa Mkoa siyo watu maalumu wa maafa wenye elimu ya masuala hayo,” amesema.
"Mara nyingi ninazungumza bungeni kuikumbusha Serikali wajibu wake namba moja wa kulinda raia. Siasa na kubezana kunapoteza maana.”
Mbatia alimtolea mfano mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi aliyeonya juu ya kivuko hicho kuwa hakikuwa katika hali nzuri, hakuna aliyejali mpaka imetokea ajali hiyo.
Na Kalunde Jamal, Dar es Salaam
Social Plugin