ALIYEUA MKEWE KWA WIVU WA MAPENZI AKAMATWA


JESHI la polisi Mkoani Pwani ,limefanikiwa kumkamata Salum Mzee Kondo (38),fundi ujenzi mkazi wa KidongoChekundu ,Bagamoyo aliyehusika na tukio la mauaji ya mkewe Mwajuma Omary (27) kisha kutoroka baada ya kutenda kosa hilo.

Mtuhumiwa huyo amekamatwa Septemba 2 mwaka huu ,Yombo Buza jijini Dar es salaam ambako alikimbilia baada ya kufanya kitendo hichoAgosti 31, 2018, saa 9 alasiri huko Kidongochekundu.

Akiweka bayana kuhusiana na tukio hilo kwa waandishi wa habari ,kamanda wa polisi mkoani Pwani (ACP) Wankyo Nyigesa alisema, mtuhumiwa alipokamatwa alikiri kutenda kosa hilo ,na kudai alichukua hatua hiyo kutokana na wivu wa kimapenzi .

Alieleza kwamba , mkewe alikuwa akichat na simu huku akiwa anacheka mwenyewe ndipo alipoamua kumnyang’anya simu na kukuta message alizokuwa akichat na mwanaume mwingine .

“Jambo hilo lilisababisha mgogoro kati yao ,ambao ulisuluhishwa na mwenyekiti wa kitongoji cha Magomeni B, lakini marehemu alishikilia kuchoshwa kuishi na mumewe huyo na kuomba kupewa talaka na mumewe aligoma kutoa talaka ” alifafanua Nyigesa .

Pamoja na hilo ,Nyigesa alisema wawili hao walikuwa na mgogoro mwingine, uliotokana na mtuhumiwa kuchukua ATM Card ya marehemu mkewe na kwenda kutoa sh.50,000 bila ridhaa yake.

Alibainisha ,jambo hilo lilimsababisha marehemu mkewe kuondoka nyumbani wanakoishi na kwenda kuishi kwa baba yake mdogo.

Kamanda huyo alieleza ,ilipofika tarehe 31 Agosti mwaka huu alimpigia simu mumewe kuhitaji fedha zake hizo ambapo mumewe alimwambia aende nyumbani kwao akachukue na mkewe huyo (marehemu)aliendelea kushikilia kutaka fedha zake na talaka ndipo mtuhumiwa kwa hasira alimkaba na kumsababisha kifo .

Baada ya kutenda kosa hilo mtuhumiwa alimfunika marehemu kwa shuka ndani ya chumba walichokuwa wakiishi na kuacha ujumbe kuwa ameua kutokana na wivu wa kimapenzi .

Kwa mujibu wa Nyigesa ,Ujumbe huo uliendelea kueleza ,mtuhumiwa nae anaenda kujiua hivyo mali zote walizoacha ni za watoto wawili waliozaa na marehemu.

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post