Mganga aliyejulikana kwa jina laYakub akitoa huduma kwa wananchi waliojitokeza kwenye soko la samaki la feri jijini Dar es Salaam Septemba 13,2018.
*Unanunua chupa ya maji anachanganya na dawa zake
*Wengine watoa ushuhuda, awekea ulinzi ili asisumbuliwe
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
BABU mwingine kama Babu wa Loliondo aibuka Dar! Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya Mganga wa kienyeji aliyetambulika kwa jina moja la Yakub kuanza kutoa huduma ya kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu kwa kutumia dawa anayoweka kwenye chupa ya maji ya kunywa.
Mganga huo ameanza kujizolea umaarufu na hasa unapofika sokoni hapo ambapo mbali ya kuwa na idadi kubwa ya watu wanaosubiri kupata dawa yake , pia wapo ambao wameitumia na kupona wamekuwa wakitoa ushuhuda kuwa wamepona.
Mwandishi wa Michuzi Blog amepata nafasi ya kushuhudia na kuona namna ambavyo watu wamejazana wakisubiri kupata huduma kutoka kwa mganga huyo.Gharama ya dawa zake ni Sh.3000.
Hata hivyo changamoto kubwa ni namna ya kumfikia hasa kwa mtu ambaye anafika eneo hilo kwa ajili ya kutaka kuzungumza naye .
Wingi wa watu umesababisha mganga huyo kulindwa na askari wa SUMA JKT katika kuhakikisha anakuwa salama wakati wote pindi anapotoa huduma zake.
Kwa mujibu wa watu ambao wamepata nafasi ya kutumia dawa za mganga huyo wamemsifu kwa madai dawa zake zinasaidia kwani wamepona.
Akizungumza jana na Michuzi Blog jijini Dar es Salaam, Said Katuma ambaye ni moja ya watu ambao wanamsaidia mganga huyo katika kutoa huduma zake anasema wameweka utaratibu mzuri utakaohakikisha wote wanaofika hapo wanapata dawa.
“Huyu mganga yupo hapa kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.Wakati anaanza kutoa huduma ya kutoa dawa watu walimpuuza.
“Lakini baada ya wale ambao wamepata nafasi ya kutumia dawa zake na kupona wamekuwa wakija kutoa shukrani.Hapo ndipo sasa watu wameanza kuamini na matokeo yake idadi ya watu imeongezeka kufuata dawa,”amesema Kaduma.
Sadick Fund ambaye naye ni miongoni mwa waliotumia dawa za mganga huyo anasema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la tumbo kujaa gesi na maumivu makali lakini baada ya kunywa dawa amepona na hana tatizo tena.
“Gharama ya dozi yake ni Sh.3000 kwa siku ya kwanza ambapo unanunua chupa ya maji ya kunywa na kisha kumkabidhi ambapo yeye anachanganya dawa na kisha unatumia mara tatu.
“Unapomaliza chupa ya kwanza na iwapo utataka kurudia chupa ya pili basi atakupa dawa bure. Kwa kweli anatusaidia sana ila hofu yetu ataanza kusumbuliwa kwani wameashaanza kumfuata fuata,”amesema.
Kwa mujibu wa watu wa eneo hilo la Feri ni kwamba mganga huyo huduma zake huanza saa nne asubuhi na wananchi wanaohitaji huduma wakifika wananunua chupa ya maji na kisha kuandika majina yao.
“Ukifika unanunua maji yanayouzwa na wauza maji na kisha chupa yako unaandika jina na kuiweka palee(anaonesha).Mganga kazi yake ni kuchanganya dawa akisaidiwa na mkewe na kisha anaita jina lililopo katika chupa,”amesema Jamila Mansur.
Hata hivyo wakati watu wanaomzungumzia mganga huyo wanasema yupo hapo zaidi ya mwezi mmoja na nusu , Meneja wa Soko la Samaki Feri alipoulizwa ni lini mganga huyo ameanza kutoa huduma amejibu kwamba ameanza kutoa huduma juzi.
Hata hivyo kinachoonekana wamemzuia mganga huyo kuzungumza na vyombo vya habari na moja ya kazi ambayo wanaifanya SUMA JKT ni kuhakikisha hazungumzi na waandishi zaidi ya watu wanaohitaji dawa tu.