Wananchi wa mtaa wa Imalilo Kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga wamechangishana fedha kwa ajili ya kuchonga barabara za kupita kwenye mtaa wao ili wapate kuvutiwa umeme kama walivyopewa masharti na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Shinyanga.
Wananchi hao wakizungumza na Malunde1 Blog leoe wakati walipokuwa wakichonga barabara za mtaa huo kupitia wanachuo cha ufundi Stadi Veta mkoani humo, walisema baada ya kuona miaka ina kwenda bila ya barabara zao kuchongwa na manispaa, ndipo wakaamua kuchangisha fedha na kuzichonga wenyewe ili wapate kuvutiwa umeme.
Walisema huu ni mwaka wa tatu sasa tangu walipoomba kuwekewa umeme katika mtaa wao, na kutokana na kushidwa kutekeleza masharti waliyopewa na TANESCO, kuwa mpaka barabara zao za mitaa zitakapochongwa na kuonyesha ramani za mipaka ndipo watavutiwa umeme huo na ndiyo maana wameamua kuchonga barabara.
Mmoja wa wananchi hao ambaye alichanguliwa kuwa Mwenyekiti wa kusimamia zoezi la uchongwaji wa barabara hizo, Florence Kihundo, alisema baada ya kuwa na shida ya umeme ndipo wakaitana kwenye kikao na kuchangisha fedha kila kaya Shilingi 25,000/-, ambapo kuna jumla ya kaya 115 lakini zilitoa kaya 20 tu na kupatikana shilingi 500,000/=.
“Baada ya kuona muitikio wa zoezi hili umekuwa mdogo, ndipo tukaandika barua kwenye chuo cha Ufundi Stadi Veta ili watupatie msaada wa mtambo (Greda), ambapo sisi tutachangia mafuta, ndipo wakakubali ombi letu ikiwa nao ni sehemu ya wanafunzi wao kujifunza kwa vitendo kuchonga barabara mpya.
Naye mwenyekiti wa mtaa huo Magdalena Mushashi, alipongeza wananchi wake kujitolea kuchangisha fedha za uchongaji wa barabara hizo kilomita moja, na kubainisha kuwa bajeti ya manispaa ya Shinyanga (2017-18) iliisha ambapo walipewa kilomita 39, na hivyo kuwaomba TANESCO watekeleze majukumu yao.
Kwa upande wake kaimu meneja wa Shirika hilo la Umeme TANESCO mkoani Shinyanga Athony Tarimo aliwatoa wasiwasi wananchi hao na kubainisha kuwa mwaka huu hautaisha lazima watakuwa tayari wameshavutiwa umeme huo, ikiwa bajeti yao ipo na wameshawekwa kwenye mpango.
Aidha Mwalimu wa Mitambo kutoka chuo hicho cha Veta Yona Elisha, ambaye aliambatana na wanafunzi kwenye uchongaji wa barabara mpya za mtaa huo, alisema wamefurahia kazi hiyo ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu kwa vitendo, ambapo wanachuo hao wataelewa vizuri masomo yao.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Imalilo kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga wakiangalia uchongwaji wa barabara kwenye mtaa wao ambapo wametumia nguvu zao wenyewe kwa kuchangishana fedha ili wapate kuvutiwa umeme kwenye mtaa huo.Picha zote na Marco Maduhu Malunde1 Blog.
Wanachuo cha Veta mkoani Shinyanga wakichonga barabara hiyo mpya ya mtaa wa Imalilo kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga, kama sehemu ya mafunzo kwao kwa vitendo ambapo wananchi wa mtaa huo wamegharamia fedha za mafuta.
Wanachuo Veta wakichonga barabara za mtaa wa Imalilo Kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga ili wapate kuvutiwa umeme.
Florence Kihundo ni Mwenyekiti aliyechaguliwa na wakazi wa mtaa huo wa Imalilo kusimamia uchongwaji wa barabara kwenye mtaa huo, ili wapate kuvutiwa umeme , kulingana na masharti waliodai kuwekewa na Tanesco ya kuchonga barabara za mtaa huo.
Uchongaji wa barabara ukiendelea.
Uchongaji wa barabara za mtaa wa Imalilo ukiendelea ambazo ni Kilomita moja.
Mwananchi Hadija Ndabi wa mtaa huo wa Imalilo akielezea furaha yao ya kukamilisha zoezi la uchongaji wa barabara za mtaa huo, ili waweze kuvutiwa umeme na Tanesco na kuwatoa kuishi kwenye giza.
Mwananchi Witness Isack akielezea namna walivyohamasika kuchangisha fedha ili kuchonga barabara za mtaa wao huo wa Imalilo kata ya Kitangili ambazo zitawafanya kupata umeme pamoja na kufungua shughuli zingine za kibiashara zitokanazo na matumizi ya umeme na hatimaye kuwaingizia kipato ikiwa mtaa huo ni mpya.
Sehemu ya barabara ya mtaa wa Imalilo Kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga ikiwa imechongwa na wanachuo kutoka Veta mkoani Shinyanga.
Picha zote na Marco Maduhu Malunde1 Blog.
Social Plugin