Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BASTOLA,PANGA VYAKUTWA KWENYE KITUO CHA KUPIGIA KURA

Matukio ya gari la mbunge kutobolewa matairi, nyumba ya mgombea kunusurika kuchomwa moto, bastola na panga kukutwa katika kituo cha kupigia kura ni miongoni mwa matukio yaliyoupamba uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani jana.

Matukio hayo yalijitokeza jana licha ya kuwapo kwa ulinzi mkali katika majimbo ya Ukonga, Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha kulikofanyika uchaguzi wa wabunge na pia kujaza nafasi za udiwani katika kata mbalimbali nchini.

Kama ilivyokuwa Monduli, jijini Dar es Salaam askari polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walionekana katika maeneo mengi ya wilaya hiyo wakiimarisha ulinzi.

Katika Jimbo la Ukonga, ukiacha askari waliotawanyika katika vituo vyote vya kupigia kura, FFU zaidi ya 20 walionekana wakiwa wameweka kambi katika kituo cha kupigia kura cha Ofisi ya Mtaa wa Kitunda A wakiwa na magari matano.

Bastola, panga kituoni

Wakati uchaguzi huo ukiendelea, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitangaza kuwashikilia watu wawili ambao hakutaka kuwataja majina kwa tuhuma za kukutwa na silaha kwenye vituo vya kupigia kura.

Alisema mtuhumiwa mmoja alikutwa na bastola aina ya glog yenye risasi 14 na mwingine alikutwa akiwa na panga.

Mambosasa alisema watuhumiwa hao waliingia vituoni kama mawakala.

“Huyu mwenye bastola alikuja na barua ambayo haina picha, lakini alipokuwa amekaa alishtukiwa na alipopekuliwa alikutwa na bastola,” alisema Mambosasa.

Akizungumzia hali ya uchaguzi, alisema ulikuwa shwari na hakukuwa na vurugu zozote.


Nyumba yanusurika

Katika tukio jingine, lilitokea nyumbani kwa mgombea udiwani wa CCM Kata ya Nsalaga - Mbeya, Mchungaji David Ngogo yalikutwa madumu ya mafuta ya petroli, hali iliyotafsiriwa kuwa kulikuwa na mpango wa kuichoma moto.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika aliyefika katika nyumba hiyo alisema, “Bado vyombo vyetu vinaendelea kuchunguza tukio hili, naomba unitafute kuanzia saa nane mchana,” alimwambia mwandishi.

Alipotafutwa muda huo alisema, “Nipo eneo la tukio siwezi kuzungumza lolote naomba uniache.”

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema hana taarifa za tukio hilo, “Ngoja nifuatilie kwanza nitakupa jibu.”

Alipotafutwa jioni, simu yake iliita bila ya kupokewa.

Waangalizi walichobaini

Baadhi ya waangalizi wa ndani wa uchaguzi katika Jimbo la Ukonga, walibainisha kuwa uelewa mdogo kwa wapigakura na wasimamizi wa vituo lilikuwa tatizo katika uchaguzi huo.

Akizungumza katika Kata ya Msongola jana, mwangalizi kutoka kituo cha Shirika la Wanawake na Vijana (Tafeyoco), Godwin Kasonya alisema wasimamizi wa vituo walikuwa wanawazuia waangalizi na waandishi wa habari kufanya kazi zao.

“Tumekwenda kituo kimoja kule Msongola, msimamizi amekataa kutoa ushirikiano kwa madai kwamba kwenye semina walizopata hawakuambiwa wafanye hivyo,” alisema.

Kasonya alisema changamoto nyingine ya kielimu waliyobaini ni baadhi ya mawakala wa chama cha NRA kujitokeza vituoni wakati chama hicho hakijasimamisha mgombea.

Hata hivyo, mwangalizi huyo alisema uchaguzi ulikwenda vizuri na ulikuwa huru na wa haki licha ya idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza.

Gari la mbunge

Gari la Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Gidarya (Chadema) limedaiwa kupigwa risasi matairi yote manne wakati akizunguka kusambaza mawakala wa vituo vya kupigia kura katika Kata ya Majengo wilaya ya Monduli.

Gidarya alisema tukio hilo lilitokea jana saa moja asubuhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’azi alisema matairi yametobolewa na kitu chenye ncha kali na kukanusha madai kwamba lilitobolewa matairi hayo kwa risasi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com