Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BOTI YAPINDUKA NA KUUA WATU WAWILI RUFIJI

Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
Watu watatu kati yao akiwemo mtoto wa miaka kumi,wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria wakitokea mashambani kupinduka wakati walipokuwa wakielekea msibani katika kijiji cha Nyaminywili ,kata ya Kipugira ,Rufiji mkoani Pwani .


Ajali hiyo imetokea baada ya boti hiyo kugonga gogo kwa chini na kusababisha kishindo hali iliyosababisha taharuki kwa abiria na kukimbilia upande mmoja hivyo boti ilipinduka na kuwafunika .


Kamanda wa polisi kanda maalum ya Rufiji,Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo majira ya saa 2 asubuhi septemba 19 mwaka huu.


Alisema boti ambayo usajili wake bado haujajulikana mali ya serikali ya kijiji cha Nyaminywili ikiendeshwa na nahodha Jumanne Bumbo (20) mkazi wa Nyaminywili ikitokea Nyaminywili mashambani kuelekea kijijini ikiwa na watu 21 wakiwemo watoto watatu ilipinduka.


Alitaja waliofariki dunia kuwa ni pamoja na Mwajuma Libeneke (26), mkazi wa Nyaminywili na mtoto wake Mwajuae Diola (10).


Mwingine ni Wastara Tumbo (24) mkazi wa Nyaminywili ambapo watu 18 waliopolewa wakiwa wapo hai.


Hata hivyo,majeruhi wote walipelekwa kituo cha afya Nyaminywili kwa matibabu zaidi ambapo baadae waliruhusiwa.


Boti hiyo imeshaopolewa majini ,miili imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa taratibu za mazishi.


Lyanga aliwaasa ,watumiaji wa vyombo vya majini kuwa makini na kuwapa maelekezo maalum wasafiri wa vyombo hivyo ili kujiepusha na majanga yanayoweza kujitokeza.


Nae mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ,wilayani Rufiji ambae pia ni mkuu wa wilaya hiyo ,Juma Njwayo alitoa rai kwa wamiliki wa boti na mitumbwi kuwa waangalifu na kubeba abiria kulingana na idadi inayotakiwa.


Alisema yeye alipata taarifa hiyo asubuhi kutoka kwa mtendaji wa kijiji hicho na ametoa pole kwa waliofikwa na misiba hiyo.


Kwa upande wake katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM ,Dk.Bashiru Ally alitoa pole kwa ndugu waliofikwa na mkasa huo.


Alieleza chama kipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha msiba .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com