CHADEMA WASHTUKIA ONGEZEKO LA VITUO VYA KUPIGIA KURA UKONGA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Ukonga, kimesema uchaguzi katika jimbo hilo unanyemelewa na jinamizi kutokana na sintofahamu ya idadi ya vituo vya kupigia kura.


Mkurugenzi wa Operesheni wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga, Singo Kigaila, akizungumza na waandishi wa habari katika ngome ya jimbo hilo, alisema mwaka 2015 kulikuwa na vituo 659 na watu waliojiandikisha walikuwa 293,000.


“Tangu mwaka 2015 hakuna uandikishaji wa wapigakura uliofanyika, haitegemewi idadi iongezeke, inawezekana kupungua kwa sababu wanaweza kuwepo waliofariki dunia.


“Vituo vinatakiwa kubakia 659 na si 675 vilivyotangazwa kuwepo katika Jimbo la Ukonga, kwa idadi hiyo kuna vituo 16 vilivyoongezeka,” alisema Kigaila.


Alisema wana wasiwasi mkubwa na vituo hivyo vilivyoongezeka sababu wanajua matatizo yaliyowahi kutokea katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika.


Kigaila alisema chama hicho kimekatia rufaa majibu waliyopewa na Tume ya Maadili kuhusu malalamiko waliyowasilisha, kwamba mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Mwita Waitara aliandika maneno katika mtandao akihamasisha waliyodai kuwa ni mauaji.


Alisema Tume iliwajibu kwamba wafuatilie Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujua kama namba hiyo iliyotumika ilikuwa ya Mwita na aliyetafsiri lugha iliyotumika kwenye mtandao awe mkalimani anayetambulika.


“Sisi kama chama hatuwezi kuiamuru TCRA kuchunguza na kutoa majibu ya namba iliyotumika kama ya Waitara ndani ya saa 48, hata tukipeleka sasa hivi, uchaguzi utamalizika na majibu hayatapatikana,” alisema.


Alisema kutafsiri lugha iliyotumika hakuhitaji mkalimani na wala kujua kama namba ya simu iliyotumika kama ni ya Waitara pia hakuhitaji uchunguzi huo kwani yeyote anaweza kujua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post