Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akizindua jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akizungumza baada ya kuzindua jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, mara baada ya kuzindua jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe kwa niaba ya Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe. Kushoto ni Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe na kulia ni Balozi Getrude Mongella.
Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe, akimwelekeza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, na Balozi Getrude Mongella mara baada ya mkuu huyo wa wilaya kuweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, na Balozi Getrude Mongella, wakisikiliza maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe, kuhusu namna muhogo unavyochakatwa
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiangalia unga wa muhogo uliofungashwa huku akipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiangalia baadhi ya wanakikundi cha Kitanga Green Voices wakiweka mihogo kwenye mashine tayari kwa kuichakata ili kupata chenga pamoja na wanga.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiangalia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kutokana na unga wa muhogo huku akipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices, Abia Magembe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, pia alipanda mti wa matunda katika eneo la kiwanda hicho kidogo kwenye Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation, Alicia Cedaba, akiwa na Mama Abia Magembe, Kiongozi wa Kikundi cha akina mama wa Kitanga Green Voices.
NA DANIEL MBEGA, KISARAWE
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, amepongeza jitihada za akina mama katika kubuni miradi ya maendeleo na kuongeza kuwa Serikali iko tayari kuunga mkono jitihada zao, na hasa katika miradi ya kilimo ambayo inaleta uhakika wa chakula.
DC Mwegelo amesema hayo Septemba 15, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe, ambacho kinamilikiwa na akinamama wapatao 30 wanaoongozwa na Ofisa Kilimo mstaafu, mama Abia Magembe.
Mkuu huyo wa wilaya aliweka jiwe hilo la msingi kwa niaba ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe.
Alisema anapongeza jitihada kubwa zilizofanywa na akina mama hao siyo tu katika kubuni miradi ya maendeleo, bali pamoja na kuwasaidia wengine na kusema kwamba, kiwanda hicho ni cha mfano ambapo kinakwenda sanjari na kauli mbiu ya Serikali ya kuifanya Tanzania ya Viwanda.
“Nawapongeza sana akina mama, pamoja na kiongozi wenu Mama Magembe, hakika hizi ni jitihada zinazotakiwa kuungwa mkono na serikali yangu itafanya kila njia kuona kwamba mnasimama,” alisema.
Aliwapongeza pia wafadhili wa Mradi wa Green Voices waliotoa mafunzo kwa akinamama 15 huko Hispania, ambapo akinamama 10 kati yao, akiwemo Mama Magembe, walianzisha miradi ya aina hiyo baada ya kurejea nchini huku wakiwafundisha akinamama wengine.
Mradi wa Green Voices, ambao unalenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira pamoja na kujikita katika uhakika wa chakula unafadhiliwa na taasisi ya Women for Africa Foundation inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Thereza de la Vega, ambapo kwa Tanzania akinamama 10 wanaendesha miradi mbalimbali katika mikoa sita.
Miradi mingine ni utengenezaji wa majiko banifu, ufugaji wa nyuki, kilimo cha uyoga, kilimo nyumba (green house) cha mboga mboga, ukaushaji wa matunda na mbogamboga kwa kutumia umeme-jua, kilimo cha matunda, kilimo cha viazi lishe pamoja na utengenezaji wa majiko ya umeme-jua.
Miradi hiyo iko katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma na Mwanza.
DC Mwegelo aliahidi kuwaunganisha akinamama wa kikundi hicho cha Kitanga Green Voices na taasisi mbalimbali za fedha ili kupatiwa mikopo isiyo na riba au yenye masharti nafuu, ambapo alisema tayari kikundi kimojawapo kilichopatiwa mafunzo na Mama Magembe tayari kilikwishapokea kiasi cha shilingi milioni moja kutoka Halmashauri ya Wilaya.
Alisema, wilaya yake ina mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata muhogo ili kutengeneza wanga (starch), lakini kwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha akina mama, anaamini kinaweza kuwa cha mfano katika kutekeleza maazimio hayo ya serikali.
“Tumepanga kuanzisha kiwanda cha kuchakata muhogo ili kutengeneza wanga, lakini kwa kuwa kiwanda hiki kipo, nadhani ni mwanzo mzuri wa kuona kwamba tunaweza kuongeza nguvu ili azma yetu itimie maana wilaya hii inaongoza kwa kuwa na mihogo mingi,” alisema.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Mtera Mwampamba, alisema kwamba muhogo na korosho ni mazao ya kipaumbele katika wilaya hiyo na kwamba ujio wa kiwanda hicho unaakisi malengo yao.
Awali, Mratibu wa Kikundi hicho, Mama Magembe, alisema kwamba, fedha walizopewa na wafadhili zilikuwa takriban shilingi milioni 12 ambazo walizitumia kununulia mashine na kujenga jengo moja, na familia yake binafsi iliamua kuchangia shilingi milioni nane ambazo zimejenga jengo la pili pamoja na kununulia matanki mawili ya kuvuna maji ya mvua.
Hata hivyo, jengo hilo la pili bado halijakamilika ambapo aliomba serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kusaidia kupatiwa mashine kubwa za kisasa pamoja na umeme.
“Mbali ya changamoto ya vitendea kazi na majengo, lakini pia kuna changamoto ya umeme ambapo tunatumia mashine zinazotumia nguvu kazi za watu, jambo linalokwamisha uzalishaji wake. Tungekuwa na umeme tunaamini kwamba tungeweza kuzalisha tani nyingi za unga wa muhogo, lakini pia tukipata mashine kubwa tunaweza kuchakata muhogo na kuusaga na shughuli nyingine zote zikaishia hapa hapa kuliko ilivyo sasa ambapo tunalazimika kubeba chenga na kwenda kusaga mjini,” alisema.
Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa maji safi na salama, hali inayokwamisha shughuli nyingi.
Hata hivyo, DC Mwegelo alisema kwamba, mpango wa kupeleka umeme kwenye kijiji hicho upo katika awamu ya tatu ya Umeme wa REA, lakini akaahidi kufuatilia ili kuona uwezekano wa awamu hiyo kuanzia kijijini hapo ili kusukuma mbele maendeleo.
Kuhusu suala la maji, alisema, hivi sasa kuna mpango wa kuleta maji wilayani Kisarawe kutoka Ruvu, lakini akasema, kwa kuwa maji yatakayozalishwa kila siku kutakuwa na ziada za lita takriban 2000, wataangalia uwezekano wa kusambaza majji hayo katika vijiji vingine kikiwemo Kijiji cha Kitanga.
Kuhusu changamoto ya masoko, DC Mwegelo aliahidi kushirikiana na akinamama hao na wadau wengine na kuhimiza kwamba, uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na muhogo ndio utakaotoa fursa ya kupatikana kwa masoko mengi.
DC Mwegelo alishuhudia bidhaa mbalimbali kama keki, maandazi, tambi, vitumbua, biskuti na chapatti ambazo zimetengenezwa kwa kutumia unga wa muhogo huku akisema kwamba, kilimo hicho kikiendelezwa siyo kitakuwa na tija kibiashara tu, bali kitakuwa na uhakika wa chakula.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, aliwashukuru wafadhili wa mradi huo na kuwapongeza akinamama wote ambao walipata mafunzo na kuja kuanzisha miradi.
Alisema kwamba, akinamama hao wameweza kuwapatia mafunzo wanawake wenzao zaidi ya 600 ambao wako katika vikundi mbalimbali na kwamba miradi mingi imeonyesha mafanikio makubwa.
Naye Balozi Getrude Mongella, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya taasisi ya Women of Africa Foundation, aliwataka wanawake kote nchini kubuni miradi endelevu na kuwahimiza wanaume kuwaunga mkono akinamama ili miradi hiyo iweze kufanikiwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa taasisi ya Women for Africa Foundation, Alicia Cedaba, alisema kwamba wamefurahishwa na mafanikio katika miradi mingi iliyoanzishwa na akinamama chini ya ufadhili wao na kwamba wataangalia uwezekano wa kuendelea kufadhili.