RC GAGUTI ALIPONGEZA JESHI LA POLISI KUKAMATA TANI 10 ZA KAHAWA ZIKISAFIRISHWA KWA MAGENDO

Mkoa  wa Kagera umeanza kupambana na wahujumu uchumi wanaosafirisha Kahawa kwa njia za magendo kwenda nchi jirani huku wakikwepa kulipa kodi za Serikali zinazotumika kuleta maendeleo ya wananchi katika mkoa.

Ni baada ya Jeshi la Polisi mkoani Kagera usiku wa kuamkia Septemba Mosi, 2018 kukamata magari mawili aina ya Fuso yenye namba T182 ARG na T424 AMY yakiwa yamepakia kahawa zilizokobolewa zaidi ya tani 10 katika kijiji cha Katarabuga kata Bwanjai yakiwa barabara kuu ya kuelekea Katoma hadi Kanyigo wilayani Missenyi mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Akikagua Kahawa hizo katika Kijiji cha Katarabuga Kata Bwanjai Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Marco Gaguti amelipongeza Jeshi la polisi mkoani Kagera kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo pamoja na ushirikiano kutoka kwa wananchi ambao kwa kiasi kikubwa walisaidia katika ukamatwaji wa kahawa hizo.

Gaguti alisema katika mkoa wa Kagera haitawezekana kuruhusu wahujumu uchumi kuendelea na vitendo vya biashara ya magendo na katika kuhakikisha hilo halifanyiki alisisititiza Kamati za Ulinzi na Usalama za kata na vijiji kuhakikisha zinatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kuwashirikisha wananchi katika maeneo yao ili wawadhibiti watu kama hao.

“Katika mkoa wetu mwaka huu 2018 tumelenga kukusanya tani 81,000 za kahawa lakini kwa vitendo hivi vya utoroshaji Kahawa kimagendo bila kufuata utaratibu wa kulipa kodi hatuwezi kufikia lengo,sisi serikali ya mkoa hatuwezi kurusu ardhi yetu itumike bure halafu mchana tunashangilia maendeleo ya nchi kumbe usiku kuna watu wanafanya biashara haramu tena kwa kutumia miundombinu yetu iliyogharamiwa na kodi za wananchi wakati wao wanakwepa kodi hizo, hiyo haikubaliki”, alisisitiza Gaguti.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustine Olomi alisema Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wanne kutokana na tukio hilo ambapo,alisema baada ya taratibu zote kukamilika Kahawa hizo zilizokamatwa zaidi ya tani 10 zitauzwa kwa njia ya mnada na fedha zikazopatikana zitaingizwa kwenye mfuko wa mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Missenyi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Alisema wananchi au wafanyabiashara ya Kahawa wanashauriwa kuachana na biashara ya magendo bali wauze Kahawa yao kwa mfumo sahihi uliowekwa na serikali ili kodi husika zilipwe,kama kuna mwananchi au mfanyabiashara anataka kuuza kahawa yake nje ya nchi ni sharti kufuata utaratibu uliopo na kulipa kodi zote za serikali na ataruhusiwa kuuza kahawa yake popote pale nje ya nchi.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Marco Gaguti akiangalia magunia ya kahawa iliyokamatwa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post