Mkurugenzi wa wa huduma za Tiba Shirikishi Dkt. Praxeda Agweyo (katikati) akiongea na wanahabari kuelezea huduma mpya waliyoianzisha tangu Novemba 2017 inahusisha utalaam wa kutumia vifaa vya radiolojia kama X-Ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound kutibu moja kwa moja ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi. Kulia ni Joan mmoja ya wagonjwa waliopatiwa matibabu na (kushoto) ni Mkuu wa Idara ya huduma za tiba radiolojia (Interventional Radiology) Dkt. Frolence Lwakatare. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mkuu wa Idara ya huduma za tiba radiolojia (Interventional Radiology) Dkt. Frolence Lwakatare (katikati) akiongea na wanahabari wakati akielezea jinsi huduma hiyo ilivyo muhimu kwa jamii ambalo amesema kuwa inapunguza hatari kwa mgonjwa maana upasuaji huwa unahatarisha maisha ya mgonjwa. Kulia ni Joan mmoja ya wagonjwa walipatiwa matibabu na Kushoto ni Daktari Bingwa wa Meno, Kinywa na Uso, Dkt. William Siang'a.
Daktari Bingwa wa Meno, Kinywa na Uso, Dkt. William Siang'a akizungumza.
Mmoja ya wangonjwa akielezea jinsi alivyotibiwa na kupona tatizo lililokuwa likimkabili. Yeye ametoa shukrani nyingi kwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuweza kumuwezesha kupata matibabu.
Wanahari wakiendelea na shughuli yao.
Moja ya wagonjwa akionekana muoneko wa kwanza kabla na baada ya matibabu.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanzisha kwa mara ya kwanza hapa nchini utoaji wa huduma za tiba radiolojia (Interventional Radiology) ambapo kabla ya uanzishwaji wake wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma hizi walikuwa wakienda nje ya nchi.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam wakati akielezea kuanzishwa wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa wa huduma za Tiba Shirikishi Dkt. Praxeda Agweyo amesema kuwa tiba hiyo inahusisha utalaam wa kutumia vifaa vya radiolojia kama X-Ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound kutibu moja kwa moja ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Amesema kuwa huduma ambazo zimeanza kutolewa kupitia njia hiyo kwa sasa ni kuondoa uvimbe kwenye sehemu ya kinywa, uso na shingoni (sclerotherapy for haemangioma and lymphangioma), kuweka mirija kwenye figo ambazo mirija ya kutoa mkojo imeziba (nephrostomy tube placement), kuzibua mirija ya nyongo iliyoziba (percutaneous trans hepatic biliary drainage) na kuzibua mirija ya uzazi iliyoziba (fallopian tube recanalization). Tiba nyingine ni kunyonya usaha ndani ya tumbo (abscesses drainage).
Ameongeza kuwa wastani wa mgonjwa mmoja kutibiwa uvimbe kwenye sehemu ya kinywa (sclerotherapy for haemangioma) inagharimu kiasi cha Tshs. 2 mil. ambapo kutokana na ugonjwa huo mgonjwa anahitaji kutibiwa hatua nne ili kukamilisha mzunguko wa tiba hiyo sawa na Tshs. 8 mil.
"Mgonjwa kama huyo alipokuwa akienda nje ya nchi ilikuwa inagharimu kiasi cha Tshs. 24 mil. kwa kila hatua moja sawa na Tshs. 96 mil. kwa hatua zote nne," amesema Dkt. Ongweyo.
Tangu kuanzishwa kwa huduma hizi Novemba 2017, jumla ya wagonjwa 45 wamenufaika kwa gharama ya Tshs. 360 mil. sawa na Tshs. 8 mil. kwa kila mgonjwa. Kama wangeenda nje ya nchi ingeigharimu Serikali kiasi cha Tshs. 4.320 Bil. sawa na Tshs. 96 mil. kwa kila mgonjwa.
"Tunamshukuru Mungu mpaka sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili imeokoa kiasi cha Tshs. 3.96 Bil. kwa kutoa huduma hiyo hapa nchini. Uwepo wa huduma hii hapa nchini utasaidia wananchi wengi kunufaika na hatimaye kupunguza mzigo wa kulipa fedha nyingi kwa matibabu huko nje," amesema Dkt. Ogweyo.
Kabla ya uanzishwaji wa huduma hizi hapa nchini, vifaa vilivyopo katika Idara ya Radiolojia kama vile X-Ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound vilikuwa vinatumika kufanya uchunguzi tu wa magonjwa lakini sasa vinatumika kutibu pia.
"Tunashukuru uongozi mzima wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuweza kuwapa madaktari wao mafunzo zaidi na kuweza kuwa wa kisasa zaidi, tulipopata mafunzo kwa madaktari wa hospitali ua Kenyatta walitufungua mengi na sasa nasi tunaweza na tunaokoa fedha za serkali," amesema Dkt. Ogweyo.
Social Plugin