Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Mathias Nyange. Jeneza lililopo kwenye picha sio lile alilokamatwa nalo.
Jeshi la Polisi Mkoani Songwe, linamshikilia mtu mmoja ambaye amekuwa akijihusisha na matukio mbalimbali ikiwemo, ujambazi, utapeli kwa kutumia nembo za freemason, akiwa na silaha aina ya Air Gun pamoja na risasi 135.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoani Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi Mathias Nyange amesema, mtuhumiwa huyo aliyejulikana kwa jina la Jerico Chifunda Msukuma, ni mkazi Nazareti Mjini Tunduma.
Mbali na kukutwa na vitu hivyo pia amekutwa na vitambulisho vinavyoonesha uraia wa nchi mbili Tanzania na Zambia ambapo anadaiwa kufanya matukio ya uhalifu kisha kukimbilia nchini Zambia.
Vitu vingine ambavyo amekutwa navyo Msukuma ni pamoja na jeneza dogo, pingu, pasi inayotumika kutapeli watu kupata fedha, mashine ya kunakilisha noti bandia, na karatasi zinazolingana ukubwa na noti ya shilingi 10,000.
Katika Hatua nyingine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu 12 wakiwa na vitu mbalimbali kama runinga na radio, ambavyo vimeibwa katika matukio mbalimbali na kwamba tayari vimetambuliwa na wamiliki.