Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, inayoongozwa na mwanasheria mkongwe na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, imeitaka Serikali kubadilisha na kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria ndogo ili ziendane na sheria mama za nchi kwani nyingi zinakinzana.
Chenge akiwasilisha bungeni jana taarifa ya uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa kwenye mkutano wa 10 na 12 wa Bunge, alisema kamati yake ilibaini baadhi ya kanuni zilizotungwa na wizara zinakwenda kinyume na masharti yaliyowekwa na sheria mama au sheria nyingine za nchi.
Alitaja baadhi ya mapungufu ya kanuni hizo kuwa ni pamoja na kuweka mikokoteni.
Alisema kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria kinasema sheria ndogo yoyote inapaswa kutokiuka masharti ya Sheria ya Bunge inayotoa mamlaka ya kutungwa kwake au sheria nyingine yoyote.
Sheria alizosema zinakinzana na sheria mama ni Sheria ya Mafuta na Gesi, Sheria ya Madini, Kanuni ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Sheria ya Mipango Miji.
Mipango Miji
Akizungumzia sheria hiyo, Chenge alisema ina masharti yanayokinzana na sheria mama ambapo katika kanuni ya 3 inayotoa tafsiri ya neno ‘vehicle’ ikihusisha vitu kama mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe, baiskeli ya matairi mawili na baiskeli ya matairi matatu (guta) ambapo tafsiri hiyo ni kinyume na ile inayotolewa na Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168.
Alisema sheria hiyo haijabainisha vifaa hivyo kuwa ni sehemu ya vyombo vya moto ambapo masuala hayo kwa namna yoyote ile hayahusiani na maudhui ya kanuni hiyo inayohusu masuala ya mipango miji.
“Kamati ilifanya uchambuzi na kubaini kanuni ya 3 inatoa tafsiri ya neno jengo kuwa inahusisha pia mabango ya matangazo na minara ya simu kinyume na tafsiri inayotolewa na sheria mama chini ya kifungu cha 2 ambayo pamoja na masuala mengine haijafafanua masuala ya mabango ya matangazo na minara ya simu,” alisema.
Mafuta
Akizungumzia sheria hiyo, Chenge alisema uchambuzi ulibaini Kanuni ya 4 (2) (b) ya kanuni hizi inampa Waziri wa Fedha jukumu la kushiriki katika majadiliano ya mikataba ya kugawana mapato katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini.
“Kamati inaona kanuni hii imemuongezea Waziri wa Fedha majukumu mapya ambayo hayatajwi katika kifungu cha 4 cha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi, sura ya 328.
“ Kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 47 vya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, majukumu ya yanayoainishwa na kanuni husika yanapaswa kutekelezwa na Waziri wa Nishati, TPDC na PURA kwa niaba ya Serikali ambapo majukumu haya hayaingiliani na yale ya Waziri wa Fedha chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi,” alisema.
Madini
Kuhusu Sheria ya Madini, Chenge alisema kamati imebaini dosari katika kanuni ya 3 inayotoa tafsiri ya neno Kampuni ya Mzawa/Wazawa kuwa ni ile inayomilikiwa kwa asilimia 51 na Mtanzania/Watanzania na ina asilimia 80 ya Watanzania katika nafasi za watendaji wa juu.
“Tafsiri inayotolewa katika kanuni hii haipo katika Sheria ya Makampuni Sura ya 212 ambayo ndiyo sheria mama inayosimamia masuala yote ya kampuni nchini.
“Utaratibu wa kuanzisha tafsiri mpya ya maneno ni vema ukaanzia katika Sheria Mama au Sheria nyingine ya nchi ambayo ni mahsusi kwa jambo fulani, hii itasaidia kuondoa uwezekano wa kuwa na mkanganyiko wa tafsiri za maneno mbalimbali,” alisema Chenge.
Alisema katika kanuni ya sheria hiyo pia tafsiri ya neno Kampuni ya mzawa/wazawa na Benki ya Watanzania wazawa iliyotumika katika kanuni hiyo ina ukakasi.
“Pamoja na nia njema ya wizara ya Madini ya kuweka tafsiri hizo, utekelezaji wake una changamoto na unaweza ukawa na matokeo hasi kwa kampuni kama Puma Energy ambapo Serikali inamiliki asilimia 50 ya hisa zote na kwa Benki ya NBC Ltd, ambapo Serikali inamiliki asilimia 15 ya hisa zote.
“Sheria ndogo hiyo haitambui umiliki wa Serikali wa hisa katika benki ya NBC na katika Kampuni ya Puma kuwa ni umiliki wa Watanzania na hivyo kuzikosesha kampuni hizo fursa ya kushiriki kiuchumi katika sekta ya madini.
“Halikadhalika benki na taasisi za fedha nyingi zilizosajiliwa hapa nchini ambazo hazimilikiiwi na Watanzania kwa asilimia 100 au kwa hisa nyingi zitakosa fursa ya kushiriki kwenye sekta ya madini, kamati haiamini kwamba haya ndiyo yalikuwa madhumuni ya kutungwa kwa sheria hiyo,” alisema Chenge.