Jumla ya kesi 160 za mmomonyoko wa maadili ikiwa ni pamoja na ubakaji, mimba za utotoni na ulawiti zimeripotiwa kwa kipindi cha miezi sita ikiwemo kesi ya wazazi wawili baba na mama kushirikiana kumbaka mtoto wa miaka 10.
Hayo yalibainika jana katika Kongamano la maadili lililoandaliwa na Jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Kigoma Mjini, ambapo Mkuu wa Kitengo cha Dawati la jinsia Kigoma,ASP Amina Kahando alisema kesi hizo zimeripotiwa ndani ya mwezi Januari hadi june ambapo kesi 135 ni za ubakaji , kesi 16 ni za ulawiti na kesi 19 ni za mimba za utotoni.
Alisema kesi hizo nyingi zinatokana na wazazi wengi kukimbia jukumu la malezi na kuwaachia wadada wa kazi, shule na jeshi la polisi na kupelekea watoto kutokuwa na uangalizi mzuri na kupelekea mmomonyoko wa maadili kutokea.
Hata hivyo Amina alisema sababu nyingine kubwa ni ya ushirikina na baadhi ya wazazi wamekuwa wakishiriki kuwabaka watoto wao, wakifikiri wanaweza kupata utajiri kwa kufanya hivyo jambo ambalo linasababisha watoto kushindwa kufikia malengo yao kutokana na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.
Alisema mpaka sasa kuna watu wamefikishwa mahakamani na wengine wamefungwa kutokana na kesi hizo na wanaendelea kuwaonya na kuwaasa wazazi kuwa makini na malezi yao ilikuepusha vitendo vya ukatili kwa watoto.
Aliongeza kuwa makosa mengine dhidi ya maadili ni vijana wengi wanakuwa wakitumia madawa ya kulevya na kusababisha kufanya vitendo vya ajabu na kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha mmomonyoko wa maadili.
Agnes Kunjira ni Ofisa ustawi Manispaa ya Kigoma Ujiji, alisema kesi nyingi anazo kutana nazo ni za watoto wengi kutelekezwa na wazazi wao pamoja na kesi za ubakaji na ulawiti na mimba za utotoni kutokana na watoto wanaanza ngono kabla ya umri wao kutokana na malezi ya wazazi wao.
Alisema mpaka sasa wamepokea watoto 40 ambao wametelekezwa na wazazi wao ambao wako mtaani na wapo watoto wengi wanazagaa mtaani hawana watu wa kuwalea na hawajaenda kuripoti ofisini na wanaweza kujikuta wanaingia katika vitendo vya ukiukwaji wa maadili kwakuwa hawana mtu anayewaangalia.
Alisema wazazi wengi wa kiume wamekuwa wakiwatelekeza watoto wao na kuwaachia wazazi wa kike kulea peke yao na wao wanashindwa kulea na kusababisha malezi kuendelea kushuka na kusababisha watoto kujiingiza kwenye mambo ya ajabu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Manispaa ya Kigoma Ujiji Juma Chaurembo, alisema wameandaa kongamano la maadili kwaajili ya kutengeneza maadili kwa kuwakumbusha wazazi majukumu yao ya kulea watoto kuwa na malezi mazuri ili kulinda amani iliyopo.
Alisema kama hakuna maadili mema hata amani iliyopo inaweza kupotea kwa kuwa watoto watakosa utu na kuanza kujiingiza kwenye vitendo vya uasi, hivyo wazazi wanatakiwa kubadilika na kuwalea watoto wao katika maadili meama.
"Kwanza tulizoea kuona mtoto anahurumiwa na mzazi hata mzazi ambaye sio mzazi wake kwa kuwa mtoto ni wawote jambo hili limepungua kutokana na mmomonyoko wa maadili hivyo jukumu la malezi linatakiwa kuchukuliwa na wazazi wote ukiona mtoto anakosea muonye hata kama sio wako muonye", alisema Chaurembo.
Alisema wazazi wakichukua nafasi yao ya malezi itasaidia sana kuwalea watoto katika maadili mema na kufanya kuwa na kizazi chenye maadili mema na sio watoto waliokengeuka.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Social Plugin