Na Bertha Ismail, mwananchi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wamesema baada ya kumalizika kwa chaguzi ndogo nchini wataibuka na ajenda ya kudai haki na uhuru.
Wamesema uhuru na haki unavunjwa licha ya Katiba ya nchi kufafanua kwa kina kuhusu mambo hayo.
Wametoa kauli hiyo jana Alhamisi Septemba 13, 2018 katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea ubunge wa Chadema jimbo la Monduli, Yonas Laizer.
Akizungumza katika mkutano huo Lowassa amesema mambo yanayoendelea Monduli anatamani angekuwa na nafasi na uwezo wa kugombea tena ubunge ili kusimama kupinga vitendo vya uvunjaji wa katiba.
“Wana Monduli mambo yanayoendelea kwa sasa nchini yanahitaji Katiba Mpya tena itakayotoa adhabu kwa yeyote atakayekiuka au kwenda kinyume chake ikiwemo haya ya kuwanyima wapinzani kugombea, kuongoza au kufanya siasa kwa kuwatisha, kuwateka na kuwalaghai,” amesema Lowassa.
“Natamani ningegombea tena mngeona kama haya ningeruhusu ila kwa sababu siwezi basi naombeni mpeni kura Laizer. Nitakuwa nampa mbinu za kufanya na msikubali kuibiwa siku hiyo mkiletewa fujo wamama naombeni pigeni ukunga wa mwizi nasi tutawasaidia.”
Kwa upande wake Mbowe amesema kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, mikutano ya hadhara huku viongozi wa vyama vya siasa wakitishiwa ni uvunjwaji wa sheria, kwamba kwa sasa wanavuta kasi ya kuanzisha ajenda ya kutaka Katiba ya nchi kufuatwa.
“Rais anapoingia madarakani mbali na kuapa kwa kutumia kitabu cha dini yake lakini pia anaapa kulinda, kupigania na kutetea katiba ya nchi,” amesema Mbowe.
“Cha kushangaza ndio kwanza katiba inavunjwa ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kuonyeshwa kwa vipindi vya Bunge.”
Amesema kwa sasa hata wapinzani waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita wanatishiwa, kutekwa huku wenye mioyo mepesi wakilaghaiwa kwa fedha na madaraka.
“Wananchi tunapaswa kufahamu kuwa hakuna aliye juu ya sheria, si kiongozi wala mtawala. Haki na wajibu vinapaswa kufuatwa ikiwa ni pamoja na na wananchi kugombea na kuchaguliwa bila kujali wanawakilisha chama gani wala wao ni dini gani,” amesema.
Amesema anashangazwa na kitendo cha wagombea wa CCM katika chaguzi ndogo kutumia viongozi wa Serikali kuwapigia kampeni sambamba na kutumia magari ya Serikali.
“Baada ya uchaguzi huu tutaanzisha hoja ya kupata maelezo ya chaguzi hizi ni za kisheria au za kihuni hasa mawaziri na viongozi wa Serikali kupigia kampeni wagombea wa CCM,” amesema.
“Pia wagombea wenyewe kutumia magari ya Serikali ikiwemo analotumia mgombea ubunge wa CCM Monduli (Julius Kalanga). Gari hilo ni la mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha vijijini (kutaja aina na namba zake).”
Mbunge wa Chadema Arusha Mjini, Godbless Lema amewataka wananchi kumchagua Laizer ili afichue maovu ya Kalanga ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa tiketi ya Chadema kabla ya kutimkia CCM na kupitishwa kuwania tena ubunge.
Kwa upande wake Laizer amewataka wananchi wa Monduli kumchagua ili kurejesha huduma za maji za uhakika kama ilivyokuwa miaka ya nyuma Lowassa alipokuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Nichagueni jamani nihakikishe namuumbua Kalanga juu ya kuwagawia wananchi wasio wa Monduli ardhi ya Monduli,” amesema Laizer.
Chanzo- Mwananchi
Social Plugin